Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria Ndugu Amon Mpanju amesema moja ya majukumu ya Wizara hiyo ni
kusimamia na kuratibu upatikanaji wa huduma ya Msaada wa Kisheria hapa nchini
na jukumu hilo linatokana na dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika
kupanua wigo wa upatikanaji wa haki na kuwafikia wananchi wa pembezoni.
Mpanju
amebainisha hayo Julai 6 mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya Kamati ya
Uratibu wa Msaada wa Kisheria Mkoa wa Morogoro yaliyofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Hoteli ya Flomi Mkoani humo.
Amesema, makundi
hayo mara kadhaa yamekuwa yakikosa kupata haki zao ambalo ni takwa la kikatiba
kwa sababu tu ya hali zao za kiuchumi na kwamba Serikali lazima iondoe hali
hiyo kwani kutosaidia upatikanaji wa haki kwa makundi hayo ni kutotekeleza
Katiba ipasavyo.
“sasa ili kuwe
na usawa lazima ubainishe makundi ambayo hayaifikii huduma hiyo kwa hiyo,
ukiangalia suala la huduma ya msaada wa kisheria msingi wake, mzizi wake
unatokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977”. Amesema
Mpanju.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria
Ndugu Gliffin Mwakapenje yeye alijielekeza kuihimiza Kamati za Uratibu za Mikoa
kutumia sheria ya usuluhishi ya mwaka 2020 ambayo ina mifumo inayoruhusu watu
waliokizana kumalizana njia ya maridhiano badala ya kupelekena polisi au
mahakamani ili kupunguza gharama kwa wahusika wenyewe na Serikali kwani
itapunguza pia idadi ya wafungwa magerezani.
Huku Bi. Grace
Makwinya ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Rasilimali Watu katika
Wizara hiyo akieleza majukumu ya Kamati za Uratibu za Mikoa kuwa ni pamoja na
kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto, makundi maalum na jamii nzima
hususan wale waasio na uwezo katika kutafuta haki zao.
Aidha, Bi Grace
amezitaka Kamati hizo kuwa wazi katika utendaji wao wa kazi, kufanya kazi bila
upendeleo wala ubaguzi kwa kutumia kigezo chochote kiwe cha hali, jinsia dini
au kisiasa.
Nao washiriki wa
Kikao hicho wametoa maoni yao namna ya kuimarisha Kamti hizo akiwemo Dkt.
Thobias Mnyasenga ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ambaye ametaka
kuwepo umakini katika kufanya maridhiano kwa kuwa makosa mengine hayatakiwi
kufanyiwa maridhiano ikiwemo ubakaji badala yake makosa kama hayo lazima kuviachia
vyombo vya kisheria.
Naye Bi.
Marcelina Kibena ambaye ni Mjumbe wa Kamati hiyo ya Uratibu wa Msaada wa
Kisheria ambaye pia ni kiongozi kwenye shirika la Mtandao wa Vikundi vya
Wakulima Tanzania – MVIWATA amesema ili Kamati hiyo iweze kufanya kazi yake
inavyotakiwa hususan katika kutatua migogoro, ni vema matamko ya wanasiasa hapa
nchini yawe yanaendana na mabadiliko ya sheria kwa wakati uliopo.
Kamati za
Uratibu ngazi ya Mikoa zimeundwa baada ya kuona kuna umuhimu wa uwepo wa
Uratibu wa wadau wanaojishughulisha na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria
kwenye mikoa huku lengo lake hasa likiwa ni kuwasaidia wananchi kupata haki zao
za kimsingi.

Post a Comment