Mkurugenzi
wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo kutoka
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akimpa kitabu cha jinsi
ya kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza mwananchi aliyetembelea banda la taasisi hiyo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa
ya moyo wakati wa maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyomalizika
hivi karibuni katika Viwanja vya Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
14/7/2021 Serikali imeombwa kutoa uelewa wa magonjwa yasiyo ya
kuambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo kupitia vyombo vya habari,
makongamano na mikutano ya hadhara kwa kufanya hivyo watu wengi
wataepukana na magonjwa hayo.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na baadhi ya wananchi waliotembelea
banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya upimaji wa magonjwa
ya moyo wakati wa maonesho ya 45 ya kimataifa ya Dar es Salaam
yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo
barabara ya Kilwa.
Wananchi hao walisema hivi sasa watu wengi wanatembea bila ya kufahamu
afya zao zikoje na mwisho wa siku wanakufa vifo vya ghafla au kupata tatizo
kubwa la kiafya na kusema kuwa wamerogwa kitu ambacho siyo kweli.
Yusta Ngoruno mkazi wa Kimara alisema yeye alifika katika banda hilo kwa
ajili ya kupima afya anashukuru amefahamu afya yake ya moyo ikoje na ushauri wa
lishe alioupata wa jinsi ya kuepukana na magonjwa hayo atautumia kuelimisha
wengine.
“Mtaalamu kaniambia magonjwa ya moyo ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza,
kwa uelewa ambao mimi nimeipata leo hii kuhusu magonjwa haya utanisaidia
kuelimisha na wengine. Ninaiomba Serikali kupitia wataalamu wake
watoe elimu hii kwa wananchi ili nao wawe na uelewa kama nilioupata mimi
siku ya hii ya leo”,.
“Nimepata ushauri wa jinsi ya kuandaa chakula bora kwa familia yangu na
aina gani ya vyakula ninavyotakiwa kula ili niepukane na magonjwa ya moyo,
ushauri huu nitaufanyia kazi pia nitawafundisha wanawake wenzangu katika
vikundi vyetu vya maendeleo”, alisema Yusta.
Naye Mzee Ali Hamisi mkazi wa Hale mkoani Tanga alisema baada ya
kutembelea maonesho hayo akaona atembelee banda la JKCI na kupima magonjwa ya
moyo kwani hajawahi kufanya hivyo katika maisha yake.
“Nimefika katika banda hili nimepokelewa vizuri na wauguzi wamenipima
vipimo mbalimbali na kunipa ushauri nikaenda kuonana na daktari. Kwa namna ya
kipekee ninawashukuru wauguzi hawa kwani mara nyingi huwa
hatuwashukuru lakini hata ukiwa Hospitali muuguzi ndiye mtu anayekaa muda mrefu
na mgonjwa na kumpatia huduma tofauti na daktari ambaye anakaa na mgonjwa muda
mfupi”, .
“Baada ya kupima nimekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu kabla
ya hapo sikuwa nafahamu kuwa ninaugonjwa huo, nimepewa dawa ambazo nitaenda
kuzitumia ninashukuru. Ombi langu kwa Serikali ni elimu ya magonjwa haya
itolewe kwa wananchi kwa njia ya vyombo vya habari hii itawasaidia kujenga
tabia ya kupima afya zao mara kwa mara”, alisema Mzee Hamisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Tatizo Waane ambaye alikuwa katika banda hilo kwa ajili ya kutoa
huduma ya matibabu kwa wananchi alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa huduma za
ushauri, upimaji na kutibu magonjwa ya moyo mara kwa mara kwa wananchi.
“Huduma hii ya upimaji huwa ni endelevu kwani tunaitoa wakati wa
maadhimisho na maonesho mbalimbali ikiwemo siku ya shinikizo la juu la damu
Duniani, siku ya shinikizo la juu la damu Duniani, siku ya wanawake Duniani
na katika mikutano mbalimbali ambayo Taasisi inaalikwa kwenda kutoa
huduma hizo”, alisema Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya
moyo.
Taasisi hiyo katika maonesho hayo ilitoa huduma mbalimbali za ushauri na
upimaji wa magonjwa ya moyo ikiwa ni pamoja na vipimo vya kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO), mfumo wa umeme wa moyo
(Electrocardiography - ECG), urefu, uzito, kiwango cha sukari mwilini,
shinikizo la damu na vipimo vya damu ili kuangalia utendaji kazi wa ini,
figo, homa ya ini, kundi la damu na full blood picture.
Mwisho.
Post a Comment