TCU YAWATAHADHARISHA WANAODAI WANATOA HUDUMA JINSI YA KUJIUNGA NA VYUO VYA ELIMU YA JUU.

Katibu Mtendaji wa TCU Prof.Charles Kihampa (picha na mtandao)

Na Mussa Khalid Dar es salaam

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imewataka wananchi kuepuka kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya hapa nchini.

Katibu Mtendaji wa TCU Prof.Charles Kihampa ametoa wito huo leo jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa kuhusu kufunguliwa kwa dirisha la Udahili kwa waombaji wa Shahada ya kwanza katika Taasisi za elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2021/2022.

Prof Kihampa amesema kuwa waombaji wanapaswa kuzingatia masuala muhimu ikiwa ni pamoja na kusoma mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU kwa makini na kuelewa kabla ya kuanza kutuma maombi ya udahili.

Aidha Katibu huyo Mtendaji ametoa utaratibu kwa makundi mbalimbali ya uombaji huku akiwataka kujiepushwa kupotoshwa na washauri au mawakala wanaodai wanatoa huduma ya kujiunga na vyuo vikuu.

‘Waombaji wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi ni lazima wawasilishe vyeti vya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kwa vyeti vya Elimu ya Sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa vyeti vya Stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili’alisema Profesa Kihampa

Profesa Kihampa amewataka pia kuzingatia kuwasiliana na vyuo moja kwa moja na kupata taarifa za kina kuhusu program za masomo ili kujiridhisha kabla ya kutuma maombi.

Tume hiyo imesema mategemeo yao kwa wanaoweza kupata udahili kwa mwaka huu kwenye vyuo yatakuwa zaidi ya laki moja kwani udahili umeendelea kuongezeka kila mwaka.

Hata hivyo Tume hiyo imetoa wito kwa waombaji wa udahili na wananchi kuhudhuria Maonyesho ya 16 ya Elimu ya Juu,Sayansi na Teknolojia yanayotarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kuanzia Julai 26 mpaka 31 mwaka huu.

0/Post a Comment/Comments