WATANZANIA wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19,) kwa kuzingatia taratibu zinazotolewa na Wizara ya Afya pamoja na elimu ambazo zimekuwa zikitolewa na wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini.
Akizungumza na kituo cha ITV jijini Dar es Salaam Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dorothy Gwajima amesema kuwa jamii lazima ielewe kuwa hali imedhibitiwa, ila kasi ya wagonjwa inazidi kujitokeza kwa wagonjwa kulazwa katika hospitali mbalimbali.
Waziri Gwajima amesema watu wasidhani kuwa kazi itafanyika maiti zikianza kuzagaa barabarani, bali jitihada zinazofanywa na Serikali na Wizara ya Afya ni kuhakikisha jamii haipati athari na wimbi la tatu na virusi vya Corona.
"Wagonjwa wapo wanaendelea kujitokeza, maambukizi yapo, nguvu kubwa inafanyika na wataalamu wa afya ili kuzuia hali mbaya isitokee." Amesema.
Pia amewataka wananchi wasioitikia tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya kuitikia tahadhari hizo ili kuweza kuepuka na kuwaepusha wengine dhidi ya maradhi hayo.
Vilevile Gwajima amesema taratibu zinazotolewa na Wizara ya Afya zikifuatwa wimbi la tatu la maambukizi ya Corona halitaleta athari na hiyo ni pamoja na kila mmoja kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono (sanitizer,) pamoja na kuzingatia mlo kamili.

Post a Comment