Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akizungumza na Rais wa Benki ya Afrika Othman Benjelloun, kwenye
hoteli ya Sofitel Jijini Rabat, Morocco, Julai 14, 2021. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
…………………………………………………………………
Waziri Mkuu Kaasim Majaliwa ameishukuru Benki ya Afrika (BOA) kwa
jitihada zake za kuendelea kuisaidia Tanzania katika Sekta mbalimbali za
maendeleo.
Ametoa kauli hiyo jana (Jumatano Julai 14, 2021) wakati alipozungumza na
Rais wa benki hiyo Othman Benjelloun kwenye hoteli ya Sofitel, Rabat Nchini
Morocco.
Amesema kuwa uwepo wa Benki hiyo nchini Tanzania umewawezesha wananchi
kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na Benki hiyo, “kwa niaba ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan tunaishukuru
Benki ya Afrika kwa jitihada hizi”.
Aidha, Waziri Mkuu alimshauri Rais Benjelloun kuendelea kupanua wigo wa
huduma za benki hiyo nchini ili kuwafikia watanzania wengi zaidi hasa katika
sekta za Elimu, Kilimo, Mifugo na Madini.
Waziri Mkuu aliahidi kuwa ataandaa utaratibu wa kuukutanisha uongozi wa
Benki hiyo na sekta binafsi nchini Tanzania ili kuona namna watakavyoweza
kushirikiana katika kuwahudumia Watanzania.
Kwa upande wake, Rais Benjelloun amesema lengo la benki hiyo ni kuendelea
kukuza uwekezaji wake nchini Tanzania. “Sisi tupo tayari kuwekeza katika
maeneo mbayo viongozi wa taifa la Tanzania watatushauri lengo likiwa ni kutoa
mchango wetu katika kujenga uchumi”.
Naye, Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alisema kuwa benki hiyo isaidie
kukuza mahusiano ya Tanzania na Morocco katika sekta ya kilimo hasa kwenye
mazao kama vile Mchele, Tumbaku, kahawa na mazao mengine.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar Leila Muhamed Mussa amesema
yapo maeneo ya fukwe ambayo hayajawekezwa mpaka sasa hivyo ni fursa kwa
wawekezaji kuyatumia na kwamba Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefungua milango kwa wawekezaji.
Pia aliiomba benki hiyo kuona namna ya kuwawezesha wakulima wa viungo ili
waweze kufanya shughuli zao kwa tija.
Post a Comment