WAZIRI MKUU MAJALIWA MGENI RASMI SWALA IDDI LHAJI.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa 
Shekh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhad Mussa Salim alipozungumza na waandishi wa habari leo Ofisini kwake jijini Dar es salaam.

NA MUSSA KHALID DAR ES SALAAM

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika swala ya Sikukuu ya Eid-il-Adhwha itakayofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Mtoro jijini Dar es salaam July 21 mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo leo jijini Dar es salaam Shekh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhad Mussa Salim amesema sikukuu hiyo ya Eid-il-Adhwha au Idd El Hajj itaambatana na baraza la Idd kwa lengo la kuwaelimisha waumini wa Dini ya Kiislamu kuhusiana na sikukuu hiyo  kutoka kwa viongozi wao.

Shekh Alhad amewakumbusha waislamu kuwa ibada kubwa kwa siku hiyo ni kuchinja mnyama ikitokana na tukio la kihistoria ambalo Nabii Ibrahim alipotaka kumchinja mwanawe Ismail baada kuota ndoto akimchinja.

‘Ile siku ya Iddi ndio siku ya kuchinja hivyo waislamu tunatakiwa tuchinje kwani ni ibada kongwe tukikumbuka tukio la Nabii Ibrahim alipomuambia mwanawe baada ya kuona ndoto na tukumbuke ndoto za mitume ni ujumbe hivyo alimuambia mwanawe ameona amchinje na hivyo Ismail akawa tayari kuchinjwa na baba yake kilichotokea baada ya hapo Mwenyezimungu alimfidia Ismail kwa kichinjo kitukufu kwa kupelekwa kondoo maalum achinjwe badala ya ismail hivyo jambo ambalo mpaka leo tumekuwa tukichinja’amesema Shekh Alhadi

 “Swala hii ni swala ya kimataifa na sisi waislamu wa Dar es salaam tumepewa heshima hiyo kuwa ndio wenyeji wa shughuli za wala hiyo kwa mwaka huu hivyo niwakumbushe waislamu wote kuhakikisha munajitokeza kwa wingi kuswali swala hiyo’amesema Shekh Alhad

Hata hivyo Shekh huyo wa Mkoa wa Dar es salaam ametoa tahadhari kwa wenye kuchinja kuangalia na kuwachagua wanyama ambao hawana  aibu yeyote ikiwemo wenye ulemavu kama chongo,waliokatwa sikio pamoja na kukatwa mkia bali wamchinjie mola wao myama aliyemzuri.

Katika hatua nyingine Shekh Alhad ametumia fursa hiyo kuwataka  waumini wa Kiislamu kuchukua tahadhari mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa wa Uviko-19 ikiwa ni pamoja na kutopeana mikono kwani ni jambo litakalosaidia swala hiyo kuswaliwa bila yakuwa na athari yeyote.

0/Post a Comment/Comments