Na WAMJW - DSM
Viongozi wa Dini nchini wametoa matamko maalumu kwa lengo la kushirikiana na Serikali kutokomeza ukatili dhidi ya Watoto pamoja na elimu kuhusu janga la UVIKO 19.
Matamko hayo wameyatoa kupitia mkutano wa pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima Mkoani Dar es Salaam.
Askofu Alinikisa Cheyo akitoa tamko kuhusu ukatili dhidi ya Watoto kwa niaba ya Viongozi hao wa Dini wameiomba Serikali kuhakikisha watoto walioathirika na ukatili wowote wanapewa huduma za ushauri nasaha kuwasaidia kisaikolojia ili warudi katika hali ya kawaida.
"Sisi Viongozi wa Dini tutafanya kwa nafasi yetu kuwasaidia watoto hawa kiroho na kisaikolojia kwani huduma hiyo ni muhimu Kama ilivyo kwa wahanga wa madawa ya kulevya" alisema Askofu Cheyo.
Katika tamko hilo wameiomba pia Serikali kulitazama suala la ajira kwa Watoto kutokana na umasikini, kuwasaidia watoto waliomaliza darasa la Saba na kukosa fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari waingizwe kwenye mfumo wa kupata ujuzi kuwaepusha na ndoa za utotoni.
Kuhusu kuwalinda watoto dhidi ya ukatili mtandaoni, Viongozi hao wamesema watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatoa elimu kwa waamini wao.
Akiwasilisha tamko kuhusu mapambano ya UVIKO 19, kwa niaba ya Viongozi wote wa Dini waliohudhuria kikao hicho, Shekh Hassan Chizenga wamekubaliana kufuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa Afya ili kujikinga na UVIKO 19 kuanzia na kuwepo kwa vifaa vya kunawia mikono kila wakati wa kusanyiko la ibada na kupunguza muda kutozidi masaa mawili.
Viongozi hao pia wameazimia kuhakikisha waumini wote lazima kuvaa barakoa wakati wa kwenda sehemu za ibada na kukaa kwa nafasi wakati wa ibada, pia wameazimia kuanzishwa utaratibu wa kusali maeneo ya wazi iwapo nyumba za ibada zitaonekana ni finyu na kuongeza wingi wa ibada.
Aidha, wamewashauri Wazee, Watoto na wote wenye matatizo ya kiafya yanapelekea kupata maambukizi wanaweza kutokuhudhuria ibada ili kujiepusha na mikusanyiko na kuhakikisha kutoa ujumbe wa mara kwa mara ikiwemo taarifa na mafunzo kwa waamini kila wakati.
"Tunashukuru Serikali kwa kuleta chanjo nchini ikiwa ni jambo la hiari, ni Jambo jema na halipingani na misingi ya dini zetu, pamoja na juhudi hizo tunaomba Serikali ihakikishe miiko ya kujikinga izingatiwe katika maeneo mengine yote" alisisitiza Shekh Chizenga.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza katika kikao hicho amewapongeza Viongozi hao kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kupamba na masuala hayo muhimu.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa Umma ya namna ya kujikinga na UVIKO 19 hivyo Viongozi was Dini ni kiungo muhimu katika juhudi hizi kwani waamini wao kwa sehemu kubwa ndiyo wananchi wetu.
"Viongozi wa Dini wamechangia kufanya Tanzania kuwa sehemu salama na kujivunia amani iliyopo, mmeendelea kufanya kazi ya kushiriki kupambana na UVIKO 19 kwa kuendelea kuwahimiza waamini wenu kuwasikiliza wataalamu wa Afya". Amehimiza Dkt. Gwajima.






Post a Comment