Picha na Mtandaoni
Na Wakili Justine Kalebo
Katika makala iliyopita tulipata fursa ya kujifunza kuhusu SHERIA ZA BIASHARA ambapo tulijifunza kusajili kampuni. Katika makala hii tutajifunza kuhusu NAMNA YA KUSAJILI NA KUENDESHA “NGO” ambapo utafahamu uhmuhimu wa usajili wa “NGO” pamoja na mambo ya kuzingatia katika usajili. Karibu !
A: UMUHIMU WA USAJILI WA “NGO”
“NGO” au shirika lisilo la kiserikali ni miongoni mwa taasisi muhimu sana katika maendeleo ya jamii. Ni ukweli usiopingika kwamba, serikali, hata iwe na fedha kiasi gani, haiwezi kukidhi mahitaji ya kila raia, kila wakati, kila mahali na kwa kila hitaji. Tupo kwenye karne ambayo mfumo wa kipepari umeshika hatamu, japokuwa tunakiri kufuata mlengo wa kijamaa. Katika mfumo huu serikali inahitaji wadau ambao wanaweza kushirikiana nayo katika ubunifu, uibuaji, upangaji, uwezeshaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Mafanikio ya mtu hayapimwi kwa kiasi cha fedha alizo nazo, bali kwa idadi ya miradi na mipango aliyoifanikisha iliyoleta maendeleo na mafanikio kwa jamii iliyomzunguka. Mfanyabiashara asiye na mchango katika jamii inayomzunguka hawezi kudumu kwa muda mrefu. Siri kubwa kubwa ya udumifu wa biashara ni mguso na mrejesho wa biashara hiyo kwa jamii inayoizunguka. Ili kuyafanikisha haya yote ni muhimu ukawa na taasisi maalumu itakayokusaidia kutekeleza hazima yako ya kuisaidia jamii kwa ufanisi na weledi mkubwa.
Taasisi hiyo ni shirika lisilo la kiserikali “NGO” ambalo utalianzisha, si kwa kufanya biashara, bali kwa kutumia kile ulichopata kwenye biashara pamoja na vile vya wengine na kuvijumuisha pamoja kisha kuvirejesha kwa jamii katika kusimamia maendeleo yake. Japo kwa sehemu unaweza kuitumia “NGO” kuanzisha miradi mbalimbali, lakini miradi hiyo inapaswa iwe yenye lengo la kuwezesha mchakato wa kuleta maendeleo na kuisaidia jamii.
Mashirika yasiyo ya kiserikali husajiliwa na Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto kwa yale ambayo yamekusudiwa kufanya kazi kitaifa. Mashirika ambayo yamekusudiwa kufanya kazi katika Wilaya au Mkoa tu yanapaswa kusajiliwa katika ngazi hiyo husika. Usajili huu ni kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Namba 24 (2002).
B: MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA USAJILI
Kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha sheria hii, mahitaji muhimu kwa ajili ya usajili wa “NGO” ni pamoja na: Nakala 3 za katiba, Wasifu (CV) na picha 2 za kila kiongozi, Muhtasari wa kikao mlichokaa na kujadili kuanzisha shirika ukiambatana na majina na saini ya kila aliyehudhuria, Fomu ya maombi ya Usajili (NGO A Form No. 1) ambayo mtapaswa kuijaza na kuibandika stempu za shilingi 1500/=, Barua ya utambulisho kutoka kwa Mkuu wa Wilaya, Afisa Tawala au Afisa Maendeleo ya jamii wa wilaya pamoja na ada ya usajili wa shirika.
Mkishawasilisha nyaraka zenu kwa msajili yeye atazipitia na kujiridhisha kama zimekidhi vigezo vyote vinavyohitajika na baada ya hapo usajili wenu utaidhinishwa na baada ya muda mtakabidhiwa cheti cha usajili. Shirika likishasajiliwa linakuwa taasisi yenye mamlaka kamili kisheria ya kushitaki na kushitakiwa, kumiliki mali, kuuza na kununua, kuingia mikataba na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa katiba. Ni muhimu sana shirika kuwa na ofisi n na watendaji wenye sifa, kufungua akaunti benki kwa jina la shirika na kubuni miradi mbalimbali ya kuisaidia jamii. Mnapaswa kuwa wabunifu, msibweteke na kusubiri tu misaada. Anzisheni kitu tofauti kinachoigusa jamii. Msitumie miradi hiyo kujinufaisha na kwa maslahi binafsi. NGO inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa jamii endapo itatumiwa vizuri. Ni muhimu sana kufuata sheria katika uendeshaji wa NGO.
*******************************************************************************
Makala hii inapatikana kutoka katika kitabu cha JUKWAA LA SHERIA ambacho kinapatikana katika maeneo mbalimbali ya wauza vitabu nchini ikiwa ni pamoja na DAR ES SALAAM:- TPH Bookshop – mtaa wa samora, Wisdom Bookshop – Mtaa wa Samoara, MAK Bookshop - Mlimani City, Dar es salam Printers – Mtaa wa Jamhuri, Efatha Bookshop Mwenge, Ubungo Bus Terminal – kwa Joseph n.k, Pia vinapatikana mikoa yote Tanzania kwa gharama nafuu sana ya Tsh. 16,000/= tu.
Kwa Ushauri zaidi unaweza kufika katika ofisi zetu zilizopo, Dar es salaam, Posta Mpya, Jengo la Mavuno House, Ghorofa ya 1, Ofisi Na. 102B. Kwa mawasiliano zaidi au msaada wa kisheria, wasiliana nasi kwa anwani ifuatayo:-
Mkurugenzi Mkuu,
Moriah International Foundation,
Idara ya Msaada wa Kisheria,
P.O. Box 70849,
Dar es salaam.
Simu: +255 713 63 62 64 / +255 755 54 56 00 / +255 222 110 684
Email: jukwaalasheria@gmail.com / moriahlawyer@gmail.com
Facebook: Jukwaa la Sheria
Post a Comment