Baadhi Ya Wadau Wa Usafirishaji Mjini Songea
Wakiwa Kwenye Kikao Na Mkuu Wa Mkoa Waruvuma Kuzungumzia Namna Ya Kukabiliana
Na Uviko 19
Mkuu
wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ameviagiza vyombo vyote vya
usafirishaji abiria yakiwemo malori,kuhakikisha wanaweka vipukusa
mikono(sanitizers) ili kupunguza maambukizi ya UVIKO 19.
RC
Ibuge ametoa maagizo hayo wakati anafunga kikao cha wadau wa usafiri na
usafirishaji kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea ambapo pia yamepitishwa maazimio ambayo
yanahitaji utekelezaji wa pamoja.
Maazimio
na maelekezo mengine ni lazima abiria
wote wavae barakoa ambapo RC Ibuge amesisitiza
ni lazima kila mmoja kulinda afya yake na ni wajibu wa kumlinda mwingine dhidi
ya UVIKO 19.
“Ukikiuka
kumlinda mwingine maana yake umevunja sheria na ni kosa la jinai ambalo halina
tofauti na kukusudia kuua kwa hiyo sio hiari,unapopanda chombo cha moto
uhakikishe una barakoa’’,alisisitiza Ibuge.
Mkuu
wa Mkoa pia ameagiza kila stendi ya mabai ziwekwe ndoo za kutosha zenye maji
tiririka na sabuni kwenye maeneo muhimu ya kuingilia na kutoka magari na yeyote
ambaye anakiuka afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Ameagiza
elimu endelevu ya kukabiliana na UVIKO 19 itolewe na wataalam wa afya kupitia
redio za kijamii zilizopo mkoani Ruvuma ili wananchi wapate uelewa wa kutosha
kuhusu ugonjwa huo.
Hata
hivyo amesema stendi ya Mfaranyaki mjini Songea isitumike kubeba abiria kwa
sababu ya kuwepo kwa kituo cha mafuta ambacho kinaweza kusababisha maafa
makubwa kwa wananchi likitokea tatizo kama moto
Akizungumzia
utekelezaji wa sheria ya abiria kufunga mikanda na abiria wote kukaa kwenye
viti bila kusimamishwa,Brigedia Jenerali Ibuge amesema ni muhimu kuzingatia
sheria ili kupunguza msongamano kwenye
vyombo vya abiria hivyo kupunguza maambukizi.
Kuhusu
madereva bodaboda kubeba abiria zaidi ya mmoja,Mkuu wa Mkoa amesema suala hilo
halina mjadala ni marufuku kubeba mishikaki na kwamba kofia kwa abiria ni
lazima ili kujikinga.
Ametoa rai kwa wananchi wote mkoani Ruvuma kuchanja chanjo ya UVIKO 19,hata hivyo amesema chanjo hiyo ni hiari na kwamba chanjo hiyo imethibitika kitaalam inasaidia kushitua kinga ya mwili kukabiliana na UVIKO 19 hivyo kupunguza vifo au mgonjwa kuzidiwa hadi kuwekewa gasi ya kupumlia.
Post a Comment