TUNATAMBUA MCHANGO WA VIONGOZI WA DINI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI - DKT. MOLLEL

 







Na WAMJW - DSM


Serikali inatambua mchango wa viongozi wa dini katika kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini hasa katika kuhimiza utekelezaji wa afua mbalimbali za kinga kwenye jamii. 

Yameelezwa hayo leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel amesema hayo leo katika kikao cha uraghibishi (Advocacy) juu ya utekelezaji wa Dawa KJinga za Virusi vya Ukimwi (PeRP), kilichojumuisha viongozi wa dini mbalimbali nchini. 

Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Dk. Mollel amesema viongozi wa dini wana nafasi nzuri na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo. 

“Tumevuka salama kwenye hatua nyingi zote na taratibu zingine za kujikinga kwa sababu viongozi wa dini wametushika mkono wakati wote na tunajua {viongozi wa dini} mlikaa vikao na wataalamu wetu mmekubali. 

“Nimekuja hapa (kikaoni) nimemwakilisha Waziri wa Afya, Dk. Gwajima, amesema hebu nendeni tena (kwa viongozi wa dini) mnikakikishie na mniletee majibu kwamba hiki tunachokifanya tupo pamoja nao, tunapokwenda kukianzisha mpo pamoja na sisi,” amesema. 

Ameongeza “Kwa sababu najua wakati mwingine taratibu za kujikinga na ukimwi zinaleta changamoto, ni kama vile unaenda kuruhusu ngono, lakini tunawaza hili jamaa limeamua kuendelea kufanya dhambi, sasa tuliache life, si bora tu libaki salama tuendelee, kupiga injili mpaka liokoke kabla halijapata UKIMWI. 

“Kama mtu ameamua kuendelea na tabia zake za ajabu tuendelee kumuelimisha, kumueleza mistari ya mungu na wakati anakuja kukubali mungu yu hai akubali akiwa hana maambukizi, anaokoa au anakuwa sheike anakjubali dini yoyote ile, lakini anakubali akiwa salama na anazidi kuchapa neno la mungu mbele na wakija kubadilika wanakuwa na ushuhuda wa kutosha. 

“Kwa hiyo, tunatambua mchango wenu katika hili hasa inapoiofika nafasi yenu, kwa sababu tunaogopa kukanyaga dini, tunaheshimu nafasi ya dini katika nchi hii. 

“Waziri wa Afya na Rais {Samia Suluhu Hassan} wanaheshimu viongozi wa dini na Rais siku zote anatuambia fanyeni yote lakini hakikisheni mnatembea vizuri na kiongozi wa dini, isitokee nikasikia kiongozi wa dini analalamika,” amesema. 

Awali, Meneja Mpango wa Kudhibiti Ukimwi, Dk. Beatrice Mutayoba amesema kikao hicho kililenga kupokea maoni kutoka kwa viongozi hao juu ya afua ya ugawaji wa dawa kinga hiyo ya PePR kwa makundi ambayo yapo katika hatari zaidi ama ya kuambukizwa au kuambukiza UKIMWI. 

“Tayari tulishapokea mwongozo kutoka kwa WHO wa 2015 na kama nchi tukapitia tafiti zilizokwisha kufanyika tukatengeneza kikosi cha wataalamu, wakajiridhisha na tukaanza na mikoa tisa ya majaribio kuona afua hii itakubalika katika mazingira yetu, kijamii, kimila, kidesturi,” amesema. 

Ameongeza “Lakini pia kuona kama kuna uwezekano katika masuala mazima ya ‘rogisticts’ lakini tumeona ni jambo jema katika kusaidia kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI, tumetengeneza mwongozo, ulishirikisha wataalamu mbalimbali kutoka taasisi mbalimbali na kiujumla wameuridhia. 

“Viongozi wa dini tulianza nao safari, kuanzia mwanzo kabla hatujaanza kuitekeleza kwenye jamii, tukasema tukutane nao tujiridhishe tena kwamba tupo pamoja na tusikie ushauri wao tena,” amesema. 

Akizungumza hali ya maambukizi ya virusi hivyo nchini hivi sasa, amesema kiwango kimeshuka kwa kiwango cha asilimia 50 ikilinganishwa katika kipindi cha mwaka 2013 na mwaka 2016/17. 

“Maambukizi mwaka 2013 yalikuwa asilimia 11 na kufikia mwaka 2016/17 yameshuka hadi asilimia 4.5, tumepiga hatua lakini ingawa kiwango cha maambukizi kwenye jamii kimeshuka hata hivyo kwa makundi hatarishi bado kipo juu kwa karibu mara mbili zaidi,” amesema Dk. Mutayoba 

Amesema bado safari ni ndefu katika kufikia kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2025/30 akibainisha kwamba Serikali ilijiwekea lengo la kushusha kiwango cha maambukizi kufikia asilimia 77 ifikapo 2020 kutoka mwaka 2010. 

“Hata hivyo tulipojipima mwaka 2020 tuliona tumepunguza kwa asilimia 38, kwa upande wa vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 50, sasa hivi kila mwaka kuna takriban vifo 32,000 ikinganishwa na vifo 64,000 ilivyokuwa mwaka 2010,” amebainisha. 

Ameongeza “Ndiyo maana tunazidi kuongeza hizi afua kuona kwamba tutafika huko kwenye kutokomeza ukimwi ifikapo 2025 na hadi 2030 kufikia malengo ya dunia. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi hao, wameipongeza Wizara ya Afya kwa hatua mbalimbali wanazochukua katika kukabiliana na magonjwa ikiwamo UKIMWI na hata janga la CORONA na kuihakikishia Serikali kwamba ipo pamoja nayo. 

Mratibu wa Afya kutoka Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk. Yotham Mackenzie aliuomba uongozi wa Wizara hiyo kuendelea kushirikisha viongozi wa dini masuala muhimu yahusuyo afya ikiwamo pia kuwapa semina maalum kuhusu afua ya chanjo ya CORONA. 

Ombi hilo, lilikubaliwa na Naibu Waziri, Dk. Mollel ambaye alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Abel Makubi kuandaa semina wiki mbili zijazo kwa ajili ya viongozi wa dini kueleweshwa kuhusu umuhimu wa chanjo ya CORONA na kuwapeleka pia katika maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ili kujifunza kwani viongozi wa dini wakielewa watakwenda kufikisha elimu sahihi kwa jamii.

0/Post a Comment/Comments