Na WAMJW- DSM.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wananchi wote kujenga tabia ya kuwasikiliza Wataalamu wa Afya ili kuishinda vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt. Gwajima amesema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa Wataalamu wa masuala ya Afya wenye lengo la kujadili njia bora ya kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam.
"Wito wangu kwa wananchi kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza ni tuwasilikilize Wataalamu wa Afya, Wataalamu wa Afya siku zote wana lengo la kuelimisha ili wananchi wapate elimu na maamuzi sahihi kwenye Afya zao" amesema
Aliendelea kusema kuwa, yapo magonjwa yasiyoambukiza ambayo mtu anazaliwa nayo na yapo ambayo yanasababishwa na mtindo wa maisha ya wananchi wenyewe kama vile ulaji usiifaa, matumizi ya vilevi kupita kiasi, matumizi ya vyakula vya mafuta mengi, uvutaji sigara na kutofanya mazoezi.
Amesema, ulaji usiofaa ambao unapelekea viliba tumbo na utapia mlo ni moja ya visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza nchini, licha ya nchi ya Tanzania kubarikiwa kuwa na mikoa inayolima aina zote za mazao ya vyakula.
Kwa upande mwingine amesema kuwa, Serikali ilishatoa agizo kwa wanaofanya biashara zinazozalisha kelele na kusababisha magonjwa na usumbufu kwa wananchi ni lazima wafuate maelekezo yaliyotolewa na Serikali ikiwemo kuzuia kelele hizo zisiende kwa wananchi kwa kiwango kikubwa.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa, Serikali kupitia Sekta zake imejipanga kushirikiana kwa kuja na Sera na mikakati mizuri itayosaidia wananchi katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, huku akiwataka wananchi kufuata maelekezo ya Serikali ili kuondokana na magonjwa haya.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima amesema kuwa, Wizara ya Afya kupitia Kurugenzi ya tiba asili na Baraza la tiba asili na tiba mbadala inaratibu bidhaa za tiba asili zote nchini, ikiwemo bidhaa zitazosaidia kutibu magonjwa yasiyoambukiza ili kulinda Afya za wananchi.
Pia, ametoa wito kwa wananchi kutumia tiba asili zilizothibitishwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Balaza la tiba asili na tiba mbadala ili kutunza afya zao kwa kuepuka dawa zinazoweza kupelekea kupata magonjwa mengine katika miili yao.
"Mtu alikwambia kwamba nina bidhaa hizi, ndugu mnunuaji swali lako la kwanza liwe kujiuliza kama huyu bidhaa yake imethibitishwa na balaza? Cheti chake cha usajili kiko wapi? Ukikosa majibu ya maswali hayo ujue huyo mtu ni feki hana nia njema " amesema
Mbali na hayo, Dkt. Gwajima amewataka watu wote wanaohusika na tiba asili kuhakikisha wanafuata utaratibu na maelekezo ya Wizara ya Afya ili wasajiliwe na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Mwisho.



Post a Comment