Ikiwa ni siku chache zimepita tangu Klabu ya Simba izindue Application (App) yake, ikakadiriwa kuwa imeshaingiza zaidi ya shilingi milioni 200 hadi kufikia leo Septemba 8, 2021.
Simba wameingiza kiasi hicho cha fedha kutokana na idadi ya watu ambao wamejiunga katika App hiyo ambayo ili kupata huduma zake unalazimika kulipia shilingi 2,000 kwa mwezi.
Kupitia ukurasa wao wa Instagram, Simba wametangaza kuwa licha ya kuwa uzinduzi rasmi wa App hiyo ulifanyika Agosti 26, 2021 ikiwa ni siku 13 tu zimepita, kuna wafuasi zaidi ya laki moja 100,000+ wameshajiandikisha.
Ikiwa wafuasi wote hao wamelipa makato ya mwezi mmoja tu ili kuitumia App hiyo inamaanisha kuwa Simba imeingiza kiasi hicho cha fedha, lakini ikiwa kuna waliolipa malipo ya zaidi ya mwezi mmoja inamanisha malipo yaliyoingia ni zaidi ya Sh milioni 200.
Alipotafutwa Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga kuhusu hilo akasema:
“Ni kweli kiasi kilichoingia ni zaidi ya hicho, kwa kuwa wapo waliolipa malipo ya zaidi ya mwezi mmoja, wapo waliolipia malipo ya miezi sita au mwaka na kuendelea.
“Japo kuna changamoto moja ya kiufundi, wateja wanaotumia App Store kuna changamoto ya malipo kiufundi, wale wa Android ndiyo wengi, wao malipo yanaendelea kama kawaida,” alisema Kamwaga.
Ikiwa kasi hiyo itaendelea kama ilivyoanza imanaanisha itakuwa faida kubwa kwa Simba kiuchumi, hata kama idadi ya watu laki moja itabaki hivyohivyo na wakalipia ada zao za mwaka, inamaanisha kwa mwaka wataingiza zaidi ya Sh bilioni 2.4.
Na @johnharamba
#TimesFMDigital

Post a Comment