TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI) KWA KUSHIRIKIANA NA WILAYA YA KIGAMBONI KUFANYA UPIMAJI WA MAGONJWA YA MOYO BILA MALIPO KWA WANANCHI.

TAARIFA KWA UMMA

 

MAADHIMISHO YA SIKU YA MOYO DUNIANI TAREHE 29/09/2021

Katika kuadhimisha Siku ya Moyo Duniani tarehe 29/09/2021 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Wilaya ya Kigamboni  tutafanya  upimaji wa magonjwa ya Moyo bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani. Upimaji huo utafanyika katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni iliyopo eneo la Gezaulole kuanzia saa mbili (2) kamili asubuhi.

Upimaji  utafanyika kwa watoto na watu wazima. Wananchi watapimwa urefu, uzito, shinikizo la damu (BP), kiwango cha sukari mwilini, vipimo vya  kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiogram- ECG) na  moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – ECHO) na  kutoa ushauri.

 

Tutakuwa na wataalamu wa lishe ambao watatoa elimu ya lishe bora ambayo itawapa wananchi uelewa na  kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu anaweza kuyaepuka kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

Kwa wale watakaokutwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi yetu. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Tunza afya ya moyo wako ili utunze maisha ya wengine”.

Tunawaomba wananchi mtumie siku hii kujitokeza kwa wingi kupima afya zenu hii itawasaidia kujua kama mna matatizo ya moyo au la na hivyo kuanza matibabu mapema kwani asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowapokea katika Taasisi yetu mioyo yao huwa  haiko katika hali nzuri.

Aidha kama mnavyofahamu wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI hivi karibuni ilizindua mpango wa jamii shirikishi na harakishi wa uelimishaji dhidi ya chanjo ya ugonjwa wa UVIKO – 19 ambao unalenga kuwafikia wananchi walioko mbali na vituo vya afya ili wapate chanjo hiyo popote pale walipo. Tunawaomba wananchi kwa wale ambao bado hawajachanja kuitumia  nafasi hiyo kwenda kupata chanjo hii muhimu ili kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya UVIKO-19.

 

Imetolewa na :

Anna Nkinda

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

28/09/2021

0/Post a Comment/Comments