Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania Dkt Charles Msonde akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
...............................................................
NA MUSSA KHALID
Wanafunzi wa Darasa la Saba walioko Tanzania Bara katika Jumla ya shule 17,585 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi (PSLE) siku ya kesho Sept 8 na 9 mwaka huu.
Imeelezwa kuwa katika mtihani huo Jumla ya watahiniwa waliosajiliwa ni 1,132,143 ambapo kati yao wavulana ni 547,502 sawa na asilimia 48.36 na wasichana ni 584,641 sawa na asilimia 51.64.
Akitoa taarifa hiyo leo kwa vyombo vya habari jijini Dar es salaam Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania Dkt Charles Msonde amesema kati ya watahiniwa hao 1,079,943 sawa na asilimia 95.39 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 52,200 sawa na asilimia 4.61 watafanya mtihani kwa lugha ya Kingereza ambayo wamekuwa wakiitumia kujifunzia.
‘Watahiniwa wenye mahitaji maalum wapo 3,327 kati yao 108 ni wasioona,951 wenye uoni hafifu,739 wenye uziwi,358 ni wenye ulemavu wa akili na 1,171 ni wenye ulemavu wa viungo mwilini’amesema Dkt Msonde
Aidha Dkt Msonde amesema katika mtihani wa mwaka huu idadi ya masomo imeongezeka kutoka masomo matano yaliyotahiniwa mwaka 2020 kuwa masomo sita likiweko Uraia pamoja na Maadili.
Katibu Huyo Mtendaji ametoa wito kwa kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri /Manispaa/Jiji kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji wa Mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo ikiwemo kuzuia mianya inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu
Hata hivyo Baraza hilo limewataka wamiliki wa shule wote kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya Mitihani na hivyo wasiingilie majukumu ya wasimamizi wa Mitihani katika kipindi chote Cha ufanyaji wa mtihani huo.

Post a Comment