Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa
Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo OLengurumwa (katikati) Afisa
Uchachamuzi kutoka THRDC Nuru Maro (kulia) na Mkuu wa Program THRDC Leopold Mosha (kushoto) wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam
............................................................
NA MUSSA KHALID DAR ES SALAAM
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania (THRDC) umeitaka serikali kuweka mifumo bora itakayowezesha ushiriki
wa watetezi wa Haki za Binadamu na wananchi wote kuweza kushiriki katika
chaguzi na Michakato mingine ya Kidemokrasia.
Kauli hilo imetolewa leo jijini Dar es salaam
na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC Onesmo
OLengurumwa ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Demokrasia duniani
ambayo huadhimishwa kila ifikapo septemba 15 ya Kila mwaka.
Mratibu huyo amesema kuwa kwa mujibu wa
Mkataba wa Afrika kuhusu Demokrasia katika Ibara ya 4 unazitaka nchi wanachama
za umoja wa Afrika kuhakikisha kuwa zinakuza Demokrasia,Misingi ya Utawala wa
Sheria na haki za binadamu.
‘Katika kuadhimisha siku hii tunatambua
umuhimu wa Demokrasia,Utawala bora na kuheshimu haki za binadamu katika nyanja
mbalimbali ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya taifa na watu wake
yanapatikana’amesema Olengurumwa
Aidha Mratibu huyo wa THRDC amesema Tanzania
ikiwa ni moja ya nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika,Inayo
wajibu wa kuhakikisha kuwa haki za kidemokrasia na utawala bora zinazingatiwa.
‘Uwepo wa Sheria zinazominya uhuru wa
kujieleza,kupata taarifa na uhueu wa kujumuika zimeendelea kuwa mwiba mkubwa
unaokandamiza uwezekano wa kufurahia demokrasia’amesema Olengurumwa
Akitoa mapendekezo katika kuboresha hali ya
demokrasia na utawala bora nchini, Mkuu wa Program THRDC Leopold Mosha amesema
serikali isimamie misingi ya Kidemokrasia na Haki za Binadamu kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mikataba ya Kikanda na Kimataifa.
Amesema ni vyema serikali ikakubali kutia
saini Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda kuhusu demokrasia,Ikiwemo
Mkataba wa Umoja wa Afrika kuhusu Demokrasia,Uchaguzi na Utawala wa mwaka 2007.
Naye Afisa Uchachamuzi kutoka THRDC Nuru Maro
ameiomba serikali kujenga dhana ya kushauriana na kujadiliana na Makundi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na makundi ya kidini,Assasi za Kiraia,Sekta binafsi
na wananchi kwa ujumla.
Hata hivyo amependekeza kuwa serikali
ifikirie upya uamuzi wake wa kuzuia wananchi na Mashirika yasiyo ya kiserikali
kufungua kesi katika Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu na watu.
Siku ya Demokrasia ilianzishwa mwaka 2007 na Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kuyakumbusha mataifa yote umuhimu wa kusimamia mifumo na misingi duniania ambapo kwa mwaka huu dhima kuu ni’Kuimarisha uthabiti wa Kidemokrasia pindi changamoto zinapojitokeza’


Post a Comment