USAJILI WA MASHIRIKA YA KIJAMII

 


A:  Usajili wa Mashirika ya Kijamii (Societies)

Mashirika au vyama vya Kijamii 
 yasiyo vinasimamiwa na Sheria ya vyama vya kijamii (The Societies Act, ). Usajili wa mashirika haya hufanyika katika Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia ofisi ya Msajili. Ofisi hii ndiyo inapokea maombi ya usajili na kuyapitisha na kuidhinisha juu ya usajili wa shirika hilo au hapana. 

Mara baada ya kusajiliwa shirika hilo linakuwa na nguvu za kisheria za kushitaki na kushitakiwa, kuajili, kumiliki mali na kuendelea na shughuli mbalimbali za shirika hilo. Jambo la kuzingatia katika usajili wa shirika ni kwamba, shirika linapaswa kuendesha shughuli zile tu ambazo zimeelezwa katika katiba na madhumuni ya shirika hilo na si vinginevyo. Kufanya shughuli yoyote ambayo haijaelezwa katika katiba ya shirika hilo ni kufanya shughuli kinyume cha sheria. 

Viongozi wa shirika mnapaswa kuzingatia kwamba, madhumuni ya shirika yanapaswa yawe ni yale yanayoendana na katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Shirika lolote linaloanzishwa kinyume cha sheria halitapewa usajili na mamlaka inayohusika.  Shirika lolote linaloanzishwa pia halipaswi kujihusisha kwenye shughuli zozote za kisiasa, halipaswi kufanya kazi kwa misingi yoyote ya ubaguzi na linapaswa lifanye kazi sanjari na malengo, sera na sheria mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

B: Vitu Vinavyohitajika Katika Usajili

Ili kufanikiwa kusajili shirika lisilo la kiserikali unahitaji vitu vifuatavyo:- 

i Katiba; zitahitajika ziandaliwe nakala za katiba kulingana na uhitaji uliopo. Kwa kuwa katiba hiyo yaweza kuhitajika katika ngazi ya kata na wilaya kabla ya kwenda wizara ya mambo ya ndani, ni vyema zikaandaliwa nakala tano au zaidi. Mwishoni zinatakiwa zibaki nakala 3 za katiba hiyo ambazo zitapelekwa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya kuwasilisha maombi ya usajili wa shirika lenu. 

ii Fomu; Mtapaswa kujaza fomu mbili yaani SA. 1 na SA. 2 na kutoa nakala nyingine mbili za fomu hizo. Fomu hizo zinapatikana katika ofisi za Wizara ya Mambo ya ndani ofisi ya msajili wa mashirika ya kijamii. Katika fomu hizo mtahitajika kujaza taarifa mbali mbali ikiwemo; Jina la shirika, Mahali ofisi za shirika zilipo au zitakapokuwepo, anwani ya shirika, madhumuni ya shirika, na sahihi za viongozi (fomu SA. 1). 

Taarifa nyingine ni pamoja na, kama shirika lina ushirikiano wowote au ni tawi la shirika jingine lolote la kitaifa au kimataifa, aina ya wanachama wa shirika, idadi kamili ya wanachama wa shirika, tarehe shirika lilipoanzishwa, wilaya ipi ambayo shirika linaendesha shughuli zake, kama shirika lina ardhi yoyote, vyeo vya viongozi wa shirika na sahihi za viongozi (fomu SA. 2). 

iii. Muhtahsari wa Kikao cha Wanachama; Muhtahsari wa kikao cha wanachama ni muhimu sana. Muhtahsari huu ndio utakaoonyesha kwamba kikao kilikaa na kuamua kuanzisha shirika hilo, kuteua viongozi wa shirika pamoja na kupitisha rasimu ya katiba ya shirika hilo. Muhtahsari wa kikao unapaswa uonyeshe mahudhurio ya wajumbe wote wa kikao na kila aliyehudhuria kikao hicho anapaswa kusaini kuonyesha kuwa amehudhuria kikao hicho. 

iv. Orodha ya Wanachama Waasisi; Orodha ya wanachama waasisi ni muhimu sana inaweza kuwa peke yake au ikaambatishwa pamoja na muhtahsari wa kikao. Wanachama hawa waanzilishi hawapaswi kuwa chini ya 10, bali wanapaswa kuwa 10 au zaidi. 

v. Wasifu wa Viongozi wa Shirika (CV) na Picha Zao; Mnapaswa pia kuandaa wasifu wa viongozi wa shirika (CV) pamoja na picha zao (passport size). Wasifu huo wa kila kiongozi unapaswa kuwa nakala 2 au zaidi kulingana na uhitaji uliopo. Wasifu wa viongozi unapaswa kutoa taarifa muhimu za kiongozi ikiwa ni pamoja na, jina, tarehe ya kuzaliwa, mahali pa kuzaliwa, taarifa ya ndoa, anwani kamili, elimu, uzoefu wa kazi na mambo mengine muhimu. 

vi. Barua ya Kuungwa Mkono/Utambulisho; barua ya utambulisho inapaswa kutoka kwa mkuu wa wilaya ambayo ofisi ya shirika hilo ilipo. Mara nyingi barua hii inapatikana baada ya kupata utambulisho kutoka ngazi ya mtaa au kata kwenda katika ofisi ya mkuu wa wilaya. 

vii. Barua ya Maombi ya usajili kutoka kwa Uongozi wa shirika; Barua ya maombi ya usajili kutoka kwa uongozi wa shirika ni muhimu sana kwa kuwa ndio inayowasilisha maombi ya shirika katika ofisi za wizara ili ianze mchakato wa kushughulikia usajili wa shirika hilo. 

viii. Ada ya usajili; ada ya usajili inalipiwa katika ofisi za wizara ili kusaidia mchakato wa usajili upate kuendelea. Ada imegawanyika katika mafungu mbalimbali ikiwemo; ada ya maombi ya usajili, ada ya usajili, ada ya kila mwaka baada ya kusajiliwa pamoja na gharama nyinginezo. Ni muhimu kupata taarifa sahihi kutoka kwenye ofisi hizo juu ya gharama zipi mnapaswa kulipa.

Mara baada ya kujiridhisha kuwa nyaraka zote muhimu zimepatikana ikiwa ni pamoja na Ada ya usajili unaweza kupeleka nyaraka zako katika Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani Ofisi ya Msajili wa Vyama au Mashirika ya Kijamii. Ofisi ikishapokea maombi yako na malipo ya ada ya usajili itaendelea na utaratibu wa kusajili shirika hilo.  Nyaraka zitapitiwa na maafisa husika ili kujiridhisha kama mmekidhi vigezo vinavyohitajika kwa ajili ya usajili, wakishajiridhisha juu ya mahitaji yote ya usajili mchakato wa usajili utaendelea. Endapo kutaonekana kasoro zozote katika nyaraka au kitu kingine chochote, wahusika mtataarifiwa ili mfanye marekebisho kisha mchakato wa usjili uendelee.

Ni muhimu pia kutambua kuwa msajili anayo mamlaka ya kukataa usajili wa shirika lenu endapo ataona zipo sababu za msingi kisheria zinazofanya shirika lenu lisisajiliwe. Mojawapo ya sababu hizo ni: Kukosa sifa kwa viongozi watakaolisimamia shirika kulingana na aina ya shughuli mtakazofanya, malengo yenu kukinzana na sheria, nembo au malengo yenu kufanana na nembo za mashirika au taasisi za serikali na sababu nyinginezo. Kukataliwa kwa usajili huthibitishwa na barua maalumu itakayoeleza sababu za kufanya hivyo. Ili kuthibitisha usajili wa shirika hilo ofisi hiyo itatoa cheti cha usajili wa shirika hilo. Mara baada ya kupata usajili ni muhimu kuzingatia kwamba, shirika linapaswa kupeleka ripoti ya utendaji na fedha ya kila mwaka katika ofisi hizo ikiwa ni pamoja na kulipia ada na tozo mbalimbali mnazopaswa kulipa kila mwaka.  

*************************************************************************************

Makala hii inapatikana kutoka katika kitabu cha JUKWAA LA SHERIA ambacho kinapatikana katika maeneo mbalimbali ya wauza vitabu nchini ikiwa ni pamoja na DAR ES SALAAM:- TPH Bookshop – mtaa wa samora, Wisdom Bookshop – Mtaa wa Samoara, MAK Bookshop - Mlimani City, Dar es salam Printers – Mtaa wa Jamhuri, Efatha Bookshop Mwenge,  Ubungo Bus Terminal – kwa Joseph n.k, Pia vinapatikana mikoa yote Tanzania kwa gharama nafuu sana  ya Tsh. 16,000/= tu. 

Kwa Ushauri zaidi unaweza kufika katika ofisi zetu zilizopo, Dar es salaam, Posta Mpya, Jengo la Mavuno House, Ghorofa ya 1, Ofisi Na. 102B. Kwa mawasiliano zaidi au msaada wa kisheria, wasiliana nasi kwa anwani ifuatayo:-

Mkurugenzi Mkuu,
Moriah International Foundation,
Idara ya Msaada wa Kisheria,
P.O. Box 70849,
Dar es salaam.
Simu: +255 713 63 62 64 / +255 755 54 56 00 / +255 222 110 684
Facebook: Jukwaa la Sheria

1/Post a Comment/Comments

Post a Comment