JUMUIYA ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi(UWT Mkoa wa Njombe imesema hotuba iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UN ilikuwa ya kuvutia na yenye kuliheshimisha Taifa kutokana na kujawa na maneno mazuri.
Rais Samia juzi amehutubia mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani ikiwa ni mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo Machi mwaka huu, huku akimulika masuala mbalimbali kuanzia uchumi, siasa, tabianchi, COVID-19 na usawa wa jinsia.
Kutokana na hotuba hiyo, UWT Mkoa wa Njombe kupitia kwa Mwenyekiti wake Scolastika Kevela, alisema hotuba ya kiongozi huyo wa nchi imewagusa siyo tu watanzania, bali watu wa mataifa mbalimbali hasa kwa namna alivyogusia masuala muhimu yanayoendelea kigubika dunia na hasa namna alivyohimiza nguvu ya pamoja katika kuyatafutia majawabu masuala hayo.
Alisema kauli yake ya kuitaka dunia kutoyaacha nyuma mataifa yanayoendelea katika vita ya kukabiliana na janga la maambukizi ya virusi vya corona kwa kuwa inaweza kusababisha kurudi nyuma kwa maendeleo ya Dunia kwa kasi ya ajabu iwapo kila nchi itajichukulia njia yake katika kulishughulikia janga hilo, imeionyesha dunia kweli Tanzania ipo mstari wa mbele katika kukabiliana na janga hilo.
" Ukweli na hakika Rais Samia aliipangilia vizuri hotuba yake mbele ya Baraza hilo la Umoja wa Mataifa, ameanza na mguu sahihi ndani ya chombo hicho cha kimataifa hivyo kuonyesha ubora katika nafasi yake kama kiongozi wetu katika Taifa hili" alisema Scolastika
Mbali na hilo alisema hatua ya Rais Samia kugusia pia hatua anazochukua katika kumwezesha mwanamke kupanda katika ngazi mbalimbali za uongozi na hatimaye kufikia shabaha ya uwiano sawa na mwanamme ni jambo lililoonyesha dhamira yake ya dhati mbele ya Baraza hilo la kutekeleza matakwa ya kufikia malengo ya mkutano wa Beijing uliotaka uwiano sawa wa 50/50 kati ya mwanamme na mwanamke.
"Kwetu sisi wana Jumuiya ya UWT Mkoa wa Njombe amezidi kutufanya tuendelee kujivunua nafasi yake kama Rais wetu, mbali na mambo mengi na mazuri aliyoyafanya katika Taifa hili kwa kipindi kifupi tangu aapishwe amevuka na kwenda mipaka ya mbali kuionyesha Dunia kuwa Tanzania ni nchi ya namna gani" alisema Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart
Aidha wao kama wana Jumuiya hiyo kutoka Njombe watasimama naye pamoja wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake na kusisitiza kuwa Mwaka 2025 watampa miaka mingine mitano ya kuliongoza Taifa kwa kaulimbiu yao ya 'Samia mitano tena'
mwisho

Post a Comment