VYOMBO VYA SERIKALI KUJISOGEZA KARIBU NA WANANCHI NI WAJIBU WETU- DKT. GWAJIMA.

 






WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Wataalamu wa Serikali hususan wa Maendeleo ya Jamii kuwa karibu na jamii ili kutambua changamoto zao na kuweka mikakati madhubuti ya kutatua changamoto hizo katika jamii. 


Dkt. Gwajima ametoa wito huo leo, wakati leo alipomtembelea Mama Zaina Khamis mwenye watoto 6 waliokosa fursa ya kupata elimu ingali umri wao wanastahili kuendelea na masomo anaeishi na wanae katika kata ya Bangulo Gongo la mboto, baada ya kutelekezwa na mume wake aliyekuwa akiishi nae Tabata. 


"Wajibu wa vyombo vya Serikali lazima tujisogeze karibu na wananchi, wananchi watujue ili wajenge imani na sisi kwamba tupo karibu nao. Sasa hivi tuna simu za mkononi, tuna mitandao ya kijamii tuitumie vizuri " amesema Dkt. Gwajima. 


Amewataka wananchi kujiamini kwani Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mama etu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inawapenda na kuwajali na itaendelea kutatua changamoto zao hasa katika masuala ya Afya na Maendeleo ya Jamii. 


Aliendelea kusema kuwa, Mama Zaina anachukukiwa na kuhifadhiwa na Serikali kwenye makao maalum na salama katika kipindi hiki wakati watoto wake wakiendelea kufanyiwa utaratibu wa kujiunga na masomo, huku Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wakiendelea kutafuta Suluhu ya changamoto ya mzazi mwenza ili kuinusuru familia hiyo. 


Aidha, amewapongeza Waandishi wa habari na wananchi wote wanaompa taarifa mbali mbali kuhusu changamoto zinazojitokeza katika jamii na kuahidi kuendelea kutatua changamoto hizo ili Jamii inufaike na matunda ya Serikali yao inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan. 


Mbali na hayo, ametoa rai kwa wanaume kuunda vikundi vya kujadili changamoto wanazokumbana nazo na kusukuma gurudumu la Maendeleo kwa kuijenga Jamii yenye usawa na yenye kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake katika Jamii.


Ameendelea kutoa wito kwa wananchi kutojichukulia hatua mkononi pindi waingiapo kwenye mgogoro wa kufamilia, na kusisitiza kwenda katika Serikali za mitaa au ofisi za ustawi wa Jamii ili kupata Suluhu ya changamoto zao.


Mwisho

0/Post a Comment/Comments