Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akikabidhiwa ripoti ya
tathmini ya utendaji wa Mamlaka
ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa mwaka wa fedha 2020/21 na
mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa PPRA, Prof. Ninatubu Lema, katika ukumbi wa
Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.
Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akitoa agizo
kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi
na uchunguzi wa kina kwa Taasisi tano zilizofanya vibaya katika shughuli za
manunuzi ili kubaini tatizo lililosababisha Taasisi hizo kufanya vibaya kwenye
mchakato wa manunuzi baada ya kupokea ripoti ya tathmini ya utendaji
wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), jijini Dodoma.
Na: Josephine
Majura na Alice Nyange WFM - DODOMA
Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amemuagiza Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufazifanyia ukaguzi na uchunguzi wa
kina Halmashauri 4 za Wilaya na Taasisi moja ya Serikali kwa kukiuka Sheria za
Ununuzi wa Umma.
Dkt. Nchemba
alitoa maagizo hayo baada ya kupokea Ripoti ya Tathimni ya Utendaji
ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ya Mwaka wa Fedha
2020/2021, jijini Dodoma.
Dkt. Mwigulu
amesema kuwa uchunguzi lazima ufanyike ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa
watu wote watakaobainika kukiuka taratibu za ununuzi ikiwemo kutoa zabuni nje
ya mfumo wa kieletroniki wa TANePS unaotumika kuchakata zabuni.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti
Ununuzi wa Umma PPRA, Profesa Ninatubu Lema kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya
PPRA Prof. Marten Lumbanga, Taasisi tano zilizopata wastani hafifu wa kufuata
sheria taratibu na kanuni za ununuzi wa umma kuwa ni Halmashauri ya Mji Kondoa,
Halmashauri ya Mbogwe, Halmashauri ya Biharamulo, Halmashauri ya Chato na
Taasisi ya Utafiti wa Wanyama.
Aidha, Mhe.
Dkt. Nchemba alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel
Tutuba, kuziandikia waraka Taasisi 172 ambazo zimeunganishwa kwenye Mfumo wa
Ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao (TANePS) watoe sababu za kutotumia
mfumo huo katika kufanya ununuzi.
Alizitaka pia
Taasisi nunuzi zote kutumia asilimia 30 ya gharama yote ya zabuni
zinazotangazwa katika mpango wao wa ununuzi wa mwaka kwa ajili ya kuyawezesha
makundi maalumu yakiwemo ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kwa mujibu
wa Sheria ya ununuzi.
“Nimesikitika
sana baada ya kusikia kwamba kati ya Taasisi 86 mlizozikagua ni Taasisi mbili
tu ndizo zilitenga asilimia 30 katika mpango wao wa ununuzi wa mwaka kwa ajili
ya makundi maalumu,” alisisitiza Dkt. Nchemba.
Kwa upande
wake Mjumbe na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti
wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Prof. Ninatubu Lema, alisema kuwa katika Mwaka wa
Fedha 2020/2021 walifanya ukaguzi wa mikataba 8,838 ya ununuzi yenye thamani ya
Sh. trilioni 9.2 kutoka Taasisi 86.
Prof. Lema
alifafanua kuwa matokeo ya ukaguzi huo yalionesha kuwa Taasisi 130 kati ya 718
zilizounganishwa kwenye mfumo wa Ununuzi wa TANePS hazikuwasilisha mipango yao
ya ununuzi kupitia mfumo huo huku Taasisi 208 ziliwasilisha mipango yao kupitia
mfumo huo lakini zikachakata zabuni nje ya mfumo hali inayoashiria kuwepo kwa
vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Kwa upande
wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba,
alimhakikishia Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango kwamba atafuatilia maelekezo
aliyopewa na kuwawajibisha wale wote watakaobainika kuhusika na ukiukaji wa
Sheria ya ununuzi na pia kuangalia uwezo wao wa utendaji kazi na namna ya
kuwajengea uwezo.
Alisema kuwa
ni muhimu taasisi za umma zikazingatia sheria, taratibu na kanuni za ununuzi wa
umma ili kuthaminisha miradi ya maendeleo na fedha zinazotumika kwani sekta ya
ununuzi inatumia kiasi kikubwa cha Bajeti ya Serikali ambapo kwa mwaka
2020/2021, bajeti ya ununuzi ilikuwa shilingi trilioni 25 sawa na zaidi ya asilimia
75 ya Bajeti yote ya Serikali.
Bw. Tutuba
alisema kuwa Mfumo wa ununuzi wa TANePS unaleta uwazi na uwajibikaji katika
ununuzi ili fedha za umma zinazotolewa na Serikali ziweze kuleta manufaa kwa
wananchi.
Mwisho.
Post a Comment