WAZIRI UMMY AKABIDHI PIKIPIKI 74

 




Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu leo  Septemba 7, 2021 amekabidhi jumla ya pikipiki 74 kwa Makatibu Wasaidizi Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu zenye thamani ya shilingi milioni 218.


Akikabidhi pikipiki hizo Waziri Ummy amesema lengo ni kuboresha utendaji kazi wa tume  hasa katika kutembelea  walimu ili kusikiliza na kutatua changamoto  mbalimbali za kiutumishi zinazowakabili.


Ummy amewataka Makatibu Wasaidizi wa Tume kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinatumika kwa masuala ya utekelezaji wa majukumu ya kila siku na si kutumika  kama bodaboda.


Ameendelea na kusema Makatibu Wasaidizi  wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuhakikisha  wanasimamia kwa weledi  kada ya waalimu  kwa kuwa ndio wenye jukumu kubwa la kuandaa taifa letu  ili liweze kuendana na kufanikisha malengo yake katika  masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


Aidha, amewasisitiza Tume ya Utumishi wa Walimu kuendelea kusimamia maadili na wasisite kuwachukulia hatua walimu wanaokiuka maadili hasa wale walimu wanaojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.


“Simamieni maadili na nidhamu hatua zichukuliwe kama kuna maadili yamekosekana katika utumishi wa Umma hasa kwenye kada ya ualimu ambapo Taifa linategemea sababu mmeaminiwa katika kutenda haki kwa wananchi,” amesema Ummy


Waziri Ummy amesema kuwa wanawajibu wakuhakikisha wanawasikiliza, kwa karibu na kutatua changamoto zao kwa wakati  kwa kuwa wameaminiwa  kuwasimamia  kwa kufuata  sheria, taratibu na miongozo ya utumishi wa Umma.



0/Post a Comment/Comments