WAZIRI UMMY AWATAKA WALIMU WAKUU KUTOALIKA WAGENI RASMI WASIO NA MAADILI

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu akizungumza na Viongozi wa Tume ya Utumishi wa Walimu katika kikao kazi jijini Dodoma leo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu akisisitiza jambo kwenye kikao kazi chake na Tume ya Utumishi wa Walimu jijini Dodoma leo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria kukabidhi Pikipiki 75 kwa Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu ngazi ya Wilaya leo jijini Dodoma.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Pauline Mkwama akisoma taarifa ya Tume yake mbele ya Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu leo jijini Dodoma.

Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imetoa onyo kwa Walimu Wakuu wa Shule mbalimbali nchini juu ya kutoa mialiko ya wageni rasmi inayowaalika katika Shule katika Shule zao wakiwataka kuzingatia weledi wa mtu na maadili aliyonayo mbele ya Jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na Tume ya Utumishi wa Walimu jijini Dodoma leo ambapo amesema siyo kila mtu anafaa kuwa mgeni rasmi kwenye Shule bali yule mwenye weledi na taswira nzuri.

Waziri Ummy amesema hivi karibuni lilijitokeza tukio la mmoja wa Walimu Wakuu Wilayani Temeke kumualika mtu ambaye hana sifa na maadili mazuri kuwa mgeni rasmi kwenye Shule hiyo jambo ambalo siyo zuri na halipaswi kufumbiwa macho.

" Siyo tu kwa kuwa mtu anakuja kuwaunga mono katika harambee basi ndio mumualike kuwa mgeni rasmi, mtu ambaye hana taswira nzuri kwa jamii, kama ilivyofanyika kule Temeke, ukiona imetokea hivyo ujue huyo mwalimu ana shida.

Niagize Walimu Wakuu wote kuzingatia suala la Maadili ya mtu wanapoalika mgeni rasmi, nimpongeze pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kwa kulitolea tamko hilo naamini haitojitokeza tena," Amesema Waziri Ummy.

Akizungumzia suala la uhamisho wa Walimu nchini, Waziri Ummy amepiga marufuku walimu kuhamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi kwenda kingine hususani kwenye shule zilizopo maeneo ya vijijini na pembezoni bila kupeleka walimu wengine ili kutoa haki ya kupata elimu kwa wanafunzi walioko kwenye maeneo hayo.

Waziri Ummy amesema ni marufuku kuhamisha walimu vituo ya kazi bila kupeleka walimu wengine kwani unakuta mtu amepangiwa kijijini kuna walimu ambao wanahamishwa wote shule inabaki haina walimu hiyo si sawa sawa kabisa.

" Hakikisheni mnapotaka kuhamisha walimu wanne katika shule za pembezoni na vijijini mnakuwa mmeshapeleka walimu wanne ndio muwatoe hao, marufuku kutoa walimu bila kupeleka walimu hata watoto wa vijijini wanahitaji haki ya kupata elimu, kumekuwa na tabia ya walimu kupenda kupangiwa vituo vya mjini pekee hilo haliwezekani,” Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy pia amesema umefika wakati wa kuanza kuwa na mashine za Kielektroniki ili kupima mahudhurio ya Walimu lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanafundishwa kwa muda ambao umepangwa.

" Sasa hivi kumekua na wimbi kubwa la hivi vituo vya masomo ya ziada, haiwezekani mtoto wa Darasa la Pili nae anaenda 'Tuition', ili kudhibiti hali hii inabidi Walimu wetu wazingatie masaa yao ya kazi.

Inabidi tuanzishe mfumo wa kusaini wa Kielektroniki kwenye Shule zetu, tunaweza kuongea na Wakuruguenzi wetu wa Halmashauri watusaidie maana gharama zake hazizidi hata Milioni Mbili, tunaweza kuanza na Shule chache," Amesema Waziri Ummy.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy leo amekabidhi Pikipiki 75 kwa Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu TSC ngazi ya Wilaya.

Awali Katibu wa TSC, Paulina Mkwama amesema wanaishkuru serikali kutokanana kutatua changamoto za walimu, ikiwemo kulipwa madeni yao, kupandishwa madaraja na vitu vingine vya msingi ambavyo walistahiki kupewa wanapatiwa.

0/Post a Comment/Comments