Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akiishukuru Benki ya Dunia (WB) kwa kutoa
fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Maendeleo, wakati wa kikao na Makamu wa
Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez
Ghanem (wa kwanza kulia), jijini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB)
Kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, akieleza nia ya WB
kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kupambana na umasikini wakati wa
mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb)
(hayupo pichani), jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya
Kusini na Mashariki mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem (katikati) na Mwakilishi
Mkazi wa Benki ya Dunia, Mhe. Mara Warwick, wakiteta jambo baada ya mkutano wao
uliofanyika jijini Dodoma.
NA. FARIDA RAMADHAN NA JOSEPHINE
MAJURA WFM- DODOMA
Benki ya Dunia imeahidi kuisaidia
Tanzania kukabiliana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO
- 19 pamoja na kusaidia kutekeleza miradi itakayosaidia kukuza ajira kwa
vijana, kuboresha miundombinu ya afya na elimu pamoja na kuendeleza rasilimali
watu.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dodoma na
Makamu wa Rais wa Benki hiyo, Dkt. Hafez Ghanem alipokutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Aliyataja maeneo muhimu
yatakayosaidia kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira hususan kwa vijana
kuwa ni pamoja na kuwekeza katika mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano
(TEHAMA), kuimarisha sekta ya nishati ya umeme, kuboresha miundombinu ya
usafirishaji na kuimarisha sekta binafsi ili iweze kuchangia katika kutoa ajira
na kukuza uchumi wa nchi.
“Tumejadiliana mambo mengi lakini
suala la muhimu ni kuhakikisha sekta binafsi inawekewa mazingira mazuri ya
kuwekeza katika miradi itakayochochea ukuaji wa uchumi ikiwemo nishati, kukuza
ajira, pamoja na kuwekeza kwenye maeneo yatakayosaidia kuboresha afya ya mama
na mtoto pamoja na suala zima la elimu” alisema Dkt. Ghanem.
Ili kutimiza azma hiyo, Dkt. Ghanem
aliishauri Serikali kuangalia namna ya kuboresha sera na sheria zitakazochochea
wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza mitaji na technolojia
vitakavyochochea mapinduzi ya viwanda kupitia mfumo wa ushirikiano kati ya
Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita
kwa kusimamia vizuri masuala ya uchumi licha ya kuwepo kwa changamoto ya
ugonjwa wa UVIKO -19 ikilinganishwa na nchi nyingine ambapo kiwango cha ukuaji
wa uchumi wa Tanzania kimefikia wastani wa asilimia 4.6.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru benki hiyo kwa kuendelea
kushirikiana na Tanzania katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo
ikiwemo miradi mitano iliyosainiwa hivi karibuni inayogharimu zaidi ya shilingi
trilioni 1.3.
Dkt. Nchemba alisema hadi sasa benki
hiyo imewekeza zaidi ya dola bilioni 5.5 kwa ajili ya kugharamia shughuli za
maendeleo na kuishuru benki hiyo kwa ahadi ya kuendeleza ushirikiano katika
kuendeleza miradi mingine mipya ya kimkakati ikiwemo kuboresha Jiji la Dar es
Salaam pamoja na Miji mingine 45 nchini.
“Leo tumeongelea maeneo mengine
mawili ya Mkakati wa Maendeleo ambapo tumekubaliana kuweka nguvu kubwa katika
kukuza Sekta Binafsi inayolenga kutengeneza ajira nyingi kwa vijana na mpango
wa kuwawezesha wanafunzi wengi kupata elimu bila kuacha masomo” alisema Dkt.
Nchemba.
Aliihakikisha Benki ya Dunia kuwa
Tanzania itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika masuala mbalimbali ili
kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika nchi kwa haraka zaidi.
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia
(WB), Dkt. Hafez Ghanem, yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku 4 ambapo
anatarajia kukutana na viongozi mbalimbali wa nchi ili kujadiliana kuhusu
masuala ya ushirikiano kati ya Benki hiyo na Tanzania, changamoto zinazoikabili
Tanzania na fursa zilizopo ndani ya Benki hiyo.
Mwisho.
Post a Comment