Chungu kikiwa na ubani baada ya kuwekwa kwenye mti katikati (senta) ya Gamboshi leo na Askofu Sangu
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asili na tiba mbadala wilaya ya Bariadi Saguda Busaliguki katika mkutano baina yao na waganga wa kienyeji uliofanyika kijiji cha Gamboshi.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu amekutana na Waganga wa tiba asili na tiba mbadala katika kijiji cha Gamboshi kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo kuhamasisha maendeleo, imani, pamoja na kuenzi mila na desturi za kabila la wasukuma.
Askofu Sangu ameyasema hayo leo Oktoba 19,2021 katika eneo la Kigango cha Gamboshi ambapo amewataka waganga kulinda mila na desturi za kabila la wasukuma, kupiga vita ndoa za jinsia moja, utoaji mimba pamoja na mauaji ya watu wenye ulemavu
Katika hotuba yake Askofu Sangu amewataka waganga hao kuwa sehemu ya kulinda tamaduni za kabila la wasukuma ili jamii iepukane na masuala ya utoaji mimba na ndoa za jinsia moja ambazo zinadharirisha utu wa mtu na kwamba waganga hao wanatibu watu kwa asilimia kubwa sana.
‘’Mila na desturi mtazilinda ninyi, kuna mengi yanafanyika katika jamii yetu…kupitia nafasi ,mlizo nazo katika jamii, tukapandikize uhai katika maisha ya binadamu, tulinde uhai wa binadamu tangu mimba inapotungwa hadi motto anapozaliwa’’ amesema Askofu Sangu.
Amesema huko nyuma (zamani) watu wenye ulemavu wa ngozi walikuwa wakiuwawa bila hatia na kwamba lawama zote walitupiliwa waganga wa kienyeji jambo ambalo lilikuwa linaleta ukakasi katika jamii na kuonekana waganga hao hawana tija katika jamii.
Amesema tatizo la mauaji ya watu wenye ualbino lilikuwa kubwa kwa sababu walikuwa hawashirikishwi ili kutoa maoni yao wakati wanalinda mila na desturi ambapo amewataka kutunza mila nzuri na kuachana na mila potofu.
Katika hatua nyingine Askofu Sangu amewataka waganga hao kusomesha watoto kwa kuwapeleka shule, pia kuendelea kushirikiana baina ya jamii, kanisa pamoja na serikali ili kuistawisha jamii kimwili na kiroho.
Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asili wilaya ya Bariadi Saguda Busaliguki amempongeza askofu Sangu kwa kukutana na waganga hao ambao zamani walionekana hawana faida kwa jamii wakati wanatibu na kuponya wagonjwa kama zilivyo hospitali na vituo vya afya vya serikali.
Amesema tatizo la mauaji ya watu wenye ualbino liliwatesa sana waganga, lakini baada ya kukaa pamoja na serikali kwa sasa wanafanya kazi kwa amani bila bughuza yoyote huku akiwataka waganga wenzake kufanya kazi kwa kuzingatia maelekezo ya serikali.
‘’Tatizo limeisha, tulikuwa hatuna elimu na kuna baadhi yetu walikuwa wakifanya mambo tofauti, tunakuomba utusaidie tupate shule katika eneo letu sababu elimu ya watu wa Gambosho bado iko chini sana’’ amesema Busaliguki.
Kezia Masuku mkazi wa Kijiji cha Gamboshi amesema Gamboshi ni kijiji kama vijiji vingine na kwamba uvumi wa kuwa kijiji cha wachawi ulienezwa na masuala ya mbina za Wagalu na Wagika.

Post a Comment