Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika usafiri wa pikipiki (Bodaboda) katika kijiji cha Ishihimulwa wilayani Uyui mkoani Tabora wakati wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kutoa mrejesho wa utekelezaji maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Waziri wa Maji Jumaa
Aweso akizungumza wakati wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakati
ujumbe wa Mawaziri hao ukitoa mrejesho wa utekelezaji maamuzi ya Baraza la
Mawaziri kwa mkoa wa Tabora juzi kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya
ardhi katika vijiji 975.
............................................................
Na Munir
Shemweta, WANMM UYUI
Serikali imetoa sehemu
ya ardhi ya hifadhi ya Mto Igombe (Igombe River) kwa ajili ya wananchi wa
vijiji 12 vilivyopo kwenye wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Utoaji sehemu ya ardhi
hiyo ni muendelezo wa hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha
anawabakisha wananchi walioingia kwenye mgogoro wa muda mrefu na serikali kwa
kuvamia sehemu ya maeneo ya hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba na pembezoni mwa
Maeneo Chepechepe (Ardhi oevu).
Baadhi ya vijiji
vilivyonufaika na hatua hiyo ya Serikali ni pamoja na vijiji vya Mbeya,
Ishihimulwa, Gilimba, Nzubuka, Izugawima, Kingwanhoma, Usagali, Bukala pamoja
na kijiji cha Uwimate
Kamati ya Mwaziri 8
Wizara za Kisekta ikiwa wilayani Uyui mkoani Tabora juzi baadhi ya wajumbe wake
walilazimika kutumia usafiri wa pikipiki (Bodaboda) kufika sehemu ya maeneo ya
vijiji ikiwemo kijiji cha Ishihimulwa ili kutoa mrejesho wa utekelezaji Maamuzi
ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika
vijiji.
Ikiwa katika kijiji
cha Ishihimulwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta William
Lukuvi ilibidi ahutubie wakazi wa eneo hilo akiwa kwenye helikopta baada ya
wananchi kuamua kuufuata ujumbe wa Mawaziri hao eneo ilipotua badala ya sehemu
iliyopangwa kwa mkutano wa hadhara.
Aidha, Kamati ya
Mawaziri 8 pia ilifika kijiji cha Kangeme wilayani Urambo ambako huko Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwaeleza wakazi wa eneo hilo kuwa, mipaka
ya hifadhi ya msitu wa Ulyankulu iheshimiwe na wananchi waendelee kusalia
maeneo waliopo sasa.
‘’Pamoja na hifadhi ya
Msitu kusajiliwa lakini mipaka yake iheshimiwe na wananchi mbaki maeneo yenu
kama mlivyo na tutaicha timu ifanye tathmini hapa na tathmini hiyo itakuwa
shirikishii’’ alisema Waziri Lukuvi.
Mawaziri waliokuwa
kwenye msafara huo, kila mmoja alielezea mipango ya Serikali kuhusu utatuzi wa
migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975. Waziri wa Mifugo
na Uvuvi Mashimba Ndaki alisema, ni vyema wananchi wakaheshimu mipaka ya maeneo
ya hifadhi na kuacha tabia ya kuvamia maeneo hayo kwa kuwa siyo ya kuchungia
mifugo.
Waziri wa Maji Jumaa
Aweso aliwaeleza wananchi wa jimbo la Urambo kuwa, pamoja na Kamati ya Mawaziri
kujikita kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi, Serikali imesikia kilio cha muda
mrefu cha tatizo la maji kwenye jimbo la Urambo ambapo sasa jimbo hilo
litapelekewa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.
‘’Napenda niwape
salamau kutoka kwa mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan emeelekeza baada ya kilio
cha muda mrefu ule mradi wa maji wa ziwa Victoria unaopita Igunga na Nzega
pamoja na Tabora sasa utaletwa pia kwenye jimbo la Urambo’’ alisema Aweso.
Manaibu Mawaziri nao
waligusia mikakati ya Wizara zao kuhusu vijiji vilivyorasimishwa katika maeneo
ya hifadhi. Mary Masanja Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii aliwahimiza
wananchi kuhakikisha hawavamii tena hifadhi na waheshimu mipaka ya hifadhi kwa
kuacha kufanya shughuli zinazoweza kuharibu misitu.
Naibu Waziri Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande aliwaambia wakazi wa vijiji
hivyo kuwa, utunzaji mazingira siyo suala la hiari kwa kuwa wananchi wanatakiwa
kuyatunza na wasipofanya hivyo mazingira hayo yataharibu mfumo wa maisha.
Waziri wa Nchi ofisi
ya Rais Tawala na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde alisema, serikali
ya Rais Samia Suluhu Hassan mbali na kupeleka fedha za maendeleo kwenye Tarafa
na maeneo mbalimbali nchini haijalisahau jimbo la Urambo mkoani Tabora
linaloongozwa na Magreth Sitta ambapo kwa upande wa barabara imetenga takriban
bilioni 1.5 kwa ajili ya barabara za vijijini.
Mawaziri wa Wizara za
Kisekta wamemaliza ziara kwenye mkoa wa Tabora ukiwa ni mkoa wa 4 tangu kuanza
ziara yao ya kutembelea mikoa 10 na siku ya Ijumaa tarehe 15 Oktoba 2021
wanaendelea kwenye mkoa wa Mara kwa lengo la kupeleka mrejesho wa maamuzi ya
baraza la mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika
vijiji 975.
Post a Comment