Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi hiyo tarehe 26 Oktoba 2021.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo (Kushoto) alisalimiana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kongwa mkoani Dodoma Bw. White Zuberi alipokwenda kusalimia kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Kongwa alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi ya ardhi tarehe 26 Oktoba 2021. Katikati ni Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary
Makondo akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya
Kongwa mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za ardhi za
halmashauri hiyo mkoani Dodoma tarehe 26 Oktoba 2021.
..........................................
Na Munir Shemweta, WANMM KONGWA
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo
amewajia juu watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kongwa
mkoani Dodoma na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi.
Mary alitoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika
ofisi ya ardhi halmashauri ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kufuatia kuwepo
malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa kuna watumishi wa wanaodai fedha
wakati wa kutoa huduma.
Alisema, wizara yake haitasita kuchukua hatia kali kwa mtumishi yeyote
wa sekta ya ardhi atakayebainika kuwadai fedha wateja kinyume na gharama halisi
zilizowekwa na serikali kwa kisingizio cha fedha ya usafiri.
Kwa mujibu wa Mary, ofisi yake ilipokea taarifa kutoka kwa mwananchi
mmoja akidai kutakiwa kutoa kiasi cha fedha kwa ajili ya usafiri wa
kufuatilia hati jambo alilolieleza kuwa halikubaliki kwa kuwa ni kuwatesa
wananchi.
‘’Tunafuatilia kwa karibu wale wote wanaodai fedha kutoka kwa wateja
maana hamjawekwa hapa kuwakandamiza wananchi na suala hili halikubaliki’’
alisema Katibu Mkuu Mary Makondo.
Mary alisema, Wizara ya ardhi katika kuboresha huduma zake iko mbioni
kukamilisha Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call Center) ambacho kitatumika
kupokea changmoto na kero kutoka kwa wateja.
‘’Dhamana mliyopewa ninyi kama watumishi wa sekta ya ardhi ni
‘privilege’ maana ardhi inamhusu kila mtu kwa hiyo mnatakiwa kuangalia namna
bora ya kutekeleza malengo ya Wizara kwa weledi’’ alisema Mary.
Akiwa katika wilaya ya Kongwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi alipata pia fursa ya kusalimia kwenye kikao cha Baraza la
Madiwani cha Halmashauri ya Kongwa ambapo aliwaomba wajumbe wa Baraza hilo
kushirikiana na ofisi ya ardhi kuhakikisha vijiji ndani ya wilaya hiyo
vinapangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi sambamba na kuongezwa kasi ya
utoaji hati za kimila.
Wilaya ya Kongwa ina jumla ya vijiji 87 na kati ya hivyo ni vijiji 41
ndivyo vyenye Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kufanya vijiji 46
kusalia kupangiwa Mpango huo.
Kwa mujibu wa Mary Makondo Wizara ya Ardhi kwa sasa iko kwenye hatua za
kukamilisha Miradi yake mikubwa miwili ya Benki ya Dunia pamoja na mkopo wa
Benki ya Exim kwa lengo la kuhakikisha ardhi ya Tanzania inapangwa na kupimwa
na kufikia malengo ya kutoa hati 2,500, 000 katika kipindi cha miaka miwili.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye
ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa Job Ndugai alimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ardhi kwa uamuzi wake wa kuitembelea wilaya hiyo kwa lengo la kutatua
changamoto zilizojitokeza.
Hata hivyo, Ndugai aliweka wazi kuwa, moja ya changamoto kubwa kwenye wilaya hiyo ya Kongwa ni mashitaka yanayohusiana na migogoro ya ardhi ambapo aliiomba Wizara ya Ardhi kuangalia namna ya kuipatia wilaya hiyo Baraza la Ardhi la Wilaya ili kuwaondolea usumbufu wananchi kufuata huduma za Baraza Dodoma mjini.
Post a Comment