
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa
uzinduzi wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki katika eneo la
National Capital City, Jijini Dodoma leo tarehe 06 Oktoba 2021.

Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 06
Oktoba, 2021 amezindua Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma kwa niaba
ya vituo vingine 5 katika mikoa mitano hapa nchini vilivyogharimu shilingi
bilioni 51.53.
Vituo
vingine 5 vimejengwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam
vituo viwili (Temeke na Kinondoni), ambapo kituo cha Temeke kitakuwa mahsusi
kushughulikia mashauri ya kifamilia, mirathi, ndoa, talaka, malezi na matunzo.
Mhe.
Rais Samia amesema ujenzi wa kituo cha Temeke Jijini Dar es Salaam kitasaidia
kupunguza mlundikano wa kesi za namna hiyo, lakini pia kitatumika kama Chuo cha
kutoa mafunzo ya namna ya kushughulikia migogoro ya mirathi, ndoa, malezi na
matunzo nchi nzima.
Aidha,
Mhe. Rais Samia ameipongeza Mahakama kwa kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa
Vituo Jumuishi sita vya utoaji Haki (Intergrated
Justice Centres) ambao ni muhimu
katika kusimamia utoaji haki nchini, kudumisha amani hususan kupitia usuluhishi
wa migogoro mbalimbali inayotokea kwenye jamii pamoja na kukuza uchumi.
Amesema
katika vituo hivyo kutakuwa na mahakama za ngazi zote kuanzia Mahakama ya
Mwanzo, Wilaya, Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na pia eneo kwa ajili ya Mahakama ya
Rufani.
Mhe.
Rais Samia amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Mahakama kukutana na viongozi wa Wizara
ya Mawasiliano na Wizara ya Fedha kushughulikia changamoto ya gharama ya Bandwidth
ili Mahakama iweze kutekeleza majukumu
yake kimalifu kupitia mfumo wa TEHAMA.
Pia,
Mhe. Rais Samia ameagiza Mahakama ihakikishe kuwa kwenye mpango mkakati wa
miaka mitano ijayo ya maboresho ya Huduma za Utoaji Haki, mikoa 9 isiyokuwa na
Mahakama Kuu ambayo ni Njombe, Geita, Singida, Manyara, Pwani, Katavi, Songwe,
Lindi na Simiyu ipewe kipaumbele, zikiwemo kata na wilaya ambazo hazina
Mahakama.
Vilevile,
Mhe. Rais Samia amewataka wadau wote wa mfumo wa utoaji haki nchini kuzingatia
sheria, taratibu na kuongozwa na nafsi zao katika kufanya maamuzi ili kuwe na
mafanikio yanayotarajiwa.
Mhe. Rais Samia ameitaka Mahakama kushughulikia suala la ucheleweshwaji wa kesi na kumuomba Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi kuongeza usimamizi wa ubora wa maamuzi kwenye Mahakama za Mwanzo.
Post a Comment