Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza
kwenye mkesha wa sherehe za Maulid zilizofanyika msikiti wa Manispaa ya Songea
Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Ruvuma Ustaadhi Rajab Mustapher Songambele
akisoma taarifa ya MASJD NUR Manispaa ya Songea kwenye mkesha wa maulid
ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert
Ibuge
baadhi ya mashehe wakiwa kwenye mkesha wa sherehe za Maulid Msikiti wa Manispaa ya Songea
Baadhi ya waumini wa kiislam ambao wamejitokeza kwenye sherehe za mkesha
wa Maulid zilizofanyika msikiti wa Manispaa ya Songea
..........................................................
MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kumaliza chanjo ya
kwanza ya UVIKO 19 iliyotolewa na serikali ya Awamu ya sita kwa kuchanja watu 44,000.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma aliyewakilishwa na Dr.Yona Mwakabumbe wakati anatoa nasaha zake kwenye
sherehe za Maulid zilizofanyika Msikiti wa wilaya Manispaa ya Songea ambapo
mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Amesema idadi hiyo ya watu waliochanja ni
kuanzia Agosti 4 hadi Oktoba 15 mwaka huu ambapo Mkoa umefanikiwa kumaliza
chanjo zote na za ziada aina ya JJ ambazo Mkoa ulipewa.
Amewapongeza waumini wa Kiislam kwa kutoa
ushirikiano mkubwa wakati wa kutekeleza zoezi la chanjo ya kwanza ambapo
amesema watalaam wa afya walikaribishwa kutoa elimu na fursa ya kuchanja kwa
waumini.
“Baada ya kumaliza chanjo ya kwanza serikali
imetoa chanjo ya pili aina ya sinofam,Mkoa wa Ruvuma tayari tumepata mgawo ni
chanjo salama unachoma na kurudia baada ya siku 28’’,alisisitiza Dr Kanga.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi
Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Ruvuma,Ustaadh Rajabu Mustapher Songambele,amesema
MASJD NUR katika Manispaa ya Songea imetenga hekari 80 kwa ajili ya kujenga shule
ambayo itatoa elimu kuanzia chekechea hadi sekondari.
“MASJD NUR imekusudia kuwekeza kwenye elimu
ili watoto wetu wapate elimu bora na kuwa katika misingi na maadili mema kwa
sababu jamii hivi sasa imepoteza maadili’’,alisisitiza Ustaadh Songambele.
Katika hatua nyingine Katibu huyo wa BAKWATA
amesema licha ya elimu,MASJD NUR pia imekusudia ujenzi wa kituo cha afya ndani
ya Manispaa ya Songea.
Akizungumza kwenye sherehe hizo,mgeni rasmi
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewapongeza waumini wa
kiislam kwa maamuzi ya kujenga shule na kituo cha afya ambapo amesisitiza kuwa
kwa kufanya hivyo wanaisaidia serikali kuwapatia watanzania elimu na afya.
Amesema serikali ya Mkoa wa Ruvuma, inawaunga
mkono katika utekelezaji wa miradi hiyo,hata hivyo ametaka kuwepo na uwazi
namna shughuli hizo zitavyofanyika ikiwemo kujua fedha zilizoingia na matumizi
yake.
Ametoa rai kwa waumini wa kiislamu na
watanzania kwa ujumla kuenzi uzalendo na uhuru wetu kwa sababu Tanzania inayo
tunu ya kipekee ya upendo na utangamano ambayo imeifanya nchi kuwa na umoja na
amani.
“Hivi vitu viwili umoja na amani tusivichulie
kwa urahisi,nayasema haya kwa sababu kabla ya kutaja jina langu naanza na
Brigedia Jenerali, ninatambua, nimeshajionea vita maana yake nini,
nimeshashiriki, kwenye vita tuilinde amani yetu kama lulu’’,alisisitiza
Brigedia Jenerali Ibuge.
Akizungumzia mapambano dhidi ya UVIKO 19
mkoani Ruvuma,Brigedia Jenerali Ibuge amewaongeza waislamu kwa kuzingatia
tahadhari za UVIKO 19 ambapo amesema
wanafanya vizuri kwenye matumizi ya maji tiririka ambapo amesisitiza pia matumizi ya barakoa.
Hata hivyo amesema miezi miwili iliyopita
kabla ya watu kuchanja hali ya corona mkoani Ruvuma ilikuwa mbaya sana, ambapo
hivi sasa baada ya watu kuchanja hakuna mgonjwa hata mmoja anayetumia mashine
ya kupumulia.
“Idadi ya wagonjwa wanaolazwa kutokana na
kupumua imepungua mno,hali hiyo imetokana na mwamko wa kuchanja,hivyo tuendelea
kuhamasishana kuchanja chanjo inayokuja ya sinofam’’,alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa pia ametoa rai kwa waislam na watanzania wote kwa ujumla kujitokeza katika sensa ya watu na makazi ambayo inatarajia kufanyika Agosti 2022.
Post a Comment