Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa Mkoa wa Temeke Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es salaam akitoa taarifa ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai 1 mpaka Septemba
30 Mwaka huu.(picha na Mussa Khalid)
...................................
NA MUSSA KHALID,DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Temeke imesema itaendelea kuongeza kasi katika kufanya chambuzi za mifumo kwenye maeneo yanayolalamikiwa zaidi ya utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo ikiwemo sekta ya Elimu,Afya na Uchukuzi ili kuongeza ufanisi katika maeneo hayo.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Mkuu wa TAKUKURU Temeke Donasian Kessy wakati akitoa taarifa ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai 1 mpaka Septemba 30 Mwaka huu ambapo amesema katika kipindi hicho wamepokea Jumla ya malalamiko 78.
Mkuu huyo wa Takukuru amesema baadhi ya malalamilo ambayo wameyapoka katika kipindi hicho ni pamoja na 18 yamehusu rushwa ambapo kati yake 15 watoa taarifa wameelimishwa na kushauriwa na matatu yalihamishiwa katika idara nyingine.
‘Malalamiko 60 yalihusu Rushwa ambapo malalamiko 43 uchunguzi unaendelea ,malalamiko matatu uchunguzi wake umekamilika na malalamiko 14 majalada yake yamefungwa.’amesema Kessy
Aidha Kessy amesema kuwa katika kipindi cha Oktoba mpaka Disemba mwaka huu wamejipanga kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya hasa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo ambapo serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi.
‘Mapambano dhidi ya rushwa ni ya kila mwana Temeke hivyo ili kuufanya mkoa wa Temeke kuwa sehemu nzuri ya kuishi isiyokuwa na rushwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika mapambano haya’amsema Kessy
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa jiji la Dar es salaam Paul John pamoja na Denis Peter wameiomba TAKUKURU kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuzifahamu haki zao na hivyo kuepuka kushiriki katika vitendo vya Rushwa.
Hata hivyo Mkuu wa Takukuru Temeke Kessy amesema wataendelea kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania katika kutoa elimu ya Rushwa kwa vijana wenzao ili kujenga dunia iliyobora.
Post a Comment