Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari akitoa akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu kuanzia Mwezi Novemba mwaka huu mpaka April 2022
Mtaalamu wa Hali
ya Hewa TMA Rose Senyangwa (aliyesima upande wa kulia ) akitoa tathmini ya mvua
za msimu uliopita kwa kipindi cha Novemba 2020-April 2021.(picha na Mussa
Khalid)
.................................................
NA MUSSA KHALID,DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewashauri wakulima kupanda mazao na mbegu zinazokomaa ndani ya muda mfupi na zinazostahili mvua chache kama mazao ya Jamii ya mizizi na ya bustani katika msimu wa mvua Novemba 2021 Hadi April 2022 unaotarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt Agnes Kijazi ameeleza hayo leo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wanahabari akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za msimu kuanzia Mwezi Novemba mwaka huu mpaka April 2022.
Dkt Kijazi amesema kuwa kutokana na mifumo ya hali ya hewa mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya kusini mwa nchi mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma ambapo mvua zinataraji kuanza wiki ya pili ya mwezi Novemba mwaka huu.
‘Kwa upande wa Kanda ya Magharibi ambayo ni Mikoa ya Tabora, Katavi na KigomaMvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi. Mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2021 katika maeneo mengi. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2022 katika mkoa wa Katavi na wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2022 katika maeneo mengine yaliyosalia’amesema Dkt Kijazi
Aidha amesema maeneo mengi ya nchi ambayo yanapata mvua mara moja kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua ambazo ni za chini ya wastani hivyo ametoa ushauri kwa wakulima kutumia mbinu na teknolojia za kilimo za kuhifadhi maji.
‘Jamii inashauriwa kuweka mpango mzuri wa matumizi na uhifadhi wa maji na malisho, kufuga kibiashara na kuvuna mifugo kulingana na upatikanaji wa malisho na maji. Wafugaji na wavuvi wanashauriwa watumie taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani. Aidha, Wakulima wa mwani katika Mikoa ya Lindi na Mtwara wanashauriwa kupanda aina ya mbegu zinazostawi kwenye maji ya kina kirefu’amesema Dkt Kijazi.
Awali,Mtaalamu wa Hali ya Hewa TMA Rose Senyangwa ametoa tathmin ya mvua za msimu uliopita kwa kipindi cha Novemba 2020-April 2021 ambapo amesema TMA ilitabiri maeneo yanayopata mvua msimu mmoja kwa mwaka yalitabiriwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Hata hivyo Mamlaka hiyo imewakumbusha watumiaji wa taariza za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima,wafugaji,Mamlaka za wanyamapori,Mamlaka za maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.
Post a Comment