WANANCHI WAHIMIZWA KUSHIRIKI SENSA YA VYOMBO VIDOGO MAJINI YA MWAKA 2021

Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Sensa Kitaifa TASAC Kapt. Alex Katama 

Mmiliki wa chombo cha Uvuvi katika Kisiwa cha Kimoyomoyo kilichopo Wilaya ya Muleba Philemoni Jacob

Afisa Mfawidhi TASAC mkoa wa Kagera Kapt. David Chiragi

......................................

Na mwandishi wetu.

Serikali imewataka wananchi kushiriki katika Sensa ya Vyombo Vidogo Majini inayoendelea kufanyika nchini ili iweze kupata takwimu rasmi zinazohusu vyombo Vidogo vya Uvuvi na Usafirishaji Majini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati akitoa tathimini ya zoezi hilo, Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Sensa Kitaifa, Kapt. Alex Katama amesema zoezi la Sensa linaendelea vizuri ambapo hadi sasa wamesha hesabu takribani vyombo vidogo vya Uvuvi na Usafirishaji vipatavyo elf thelathini kwa Tanzania Bara.

“Tupo katika zoezi la Sensa ya Vyombo vyote vidogo ambavyo vinafanya shughuli ya Uvuvi na Usafirishaji Majini. Tunapata ushirikiano mzuri sana kutoka kwa viongozi na wananchi wa maeneo husika na hivyo hata katika maeneo ambayo bado hatujayafikia, tunaomba wananchi watoe ushirikiano” alisema Kapteni.Katama.

Katama alisema lengo kuu la Sensa ambayo imeanza kufanyika kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2021 na itakamilika tarehe 30 Oktoba, 2021 ni kupata takwimu rasmi za vyombo vidogo vya Uvuvi na Usafirishaji ili Serikali iweze kujua vipo vingapi, vinapatikana maeneo gani na vipo katika hali gani.

Alisema takwimu hizo zitasaidia kupanga mipango mbalimbali ya kuboresha hali ya uvuvi na huduma ya usafirishaji hasa kwa kutumia vyombo vidogo.

Aidha, alisema kupatikana kwa takwimu za vyombo hivyo kutasaidia kwenye uwekezaji wa viwanda vya kusindika samaki na mitambo ya kukaushia dagaa.

Ameongeza kuwa, Sensa hii itasaidia wavuvi na wasafirishaji kupata taarifa za hali ya hewa ambazo ni muhimu katika usalama wao.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Sensa katika mkoa wa Kagera, Afisa Mfawidhi wa TASAC Kapteni David Chiragi amesema mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye vyombo vingi vidogo vya Uvuvi na Usafirishaji na hivyo wanatarajia kusajili vyombo vingi zaidi ukilinganisha na maeneo mengine.

“Serikali inafanya Sensa ya Vyombo vidogo vya usafirishaji na Uvuvi majini kwa lengo la kupata takwimu ya idadi na taarifa zingine ambazo zitasaidia kwenye uratibu na usimamizi wa sekta ya uvuvi na usafirishaji majini” amesema Chiragi.

Amesema kwa upande wa TASAC, takwimu hizi zitasaidia katika udhibiti maana wataweza kujua vyombo vipo vingapi, vipo maeneo gani, na katika hali gani na vinafanya shughuli gani.

Amesema kujulikana kwa vyombo hivyo kutasaidia katika usalama wa watumiaji wa vyombo hivyo na usalama wa vyombo vyenyewe.

Chiragi amesema taarifa wanazokusanya kwenye Sensa hii ni idadi ya vyombo, usajili, mawasiliano na taarifa za makazi ya mmiliki.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Iramba Novatus Bernado amesema wamelipokea vizuri zoezi la Sensa na wananchi wa eneo lake wametoa ushirikiano vizuri kukamilisha zoezi hili muhimu la kitaifa.

Alisema kufanyika kwa Sensa hiyo kutawezesha kuimarisha sekta ya uvuvi na usafirishaji na katika masuala ya usalama pale inapotokea upotevu wa chombo kinaweza kupatikana kwa urahisi.

Ametoa wito kwa wananchi wa eneo lake kujitokeza kwa wingi kuhakikisha vyombo vyao vinahesabiwa katika Sensa hii ili Serikali iweze kupanga mipango mizuri ya kuboresha uvuvi na usafirishaji kwa kutumia vyombo vidogo.

Kwa upande wake Philemoni Jacob Mmiliki wa chombo cha Uvuvi katika Kisiwa cha Kimoyomoyo kilichopo Wilaya ya Muleba alisema Sensa hii ni nzuri kwani itawasaidia kutambulika na Serikali na hata ikitokea wamepoteza mitumbwi yao itakuwa rahisi kuipata kutokana na utambuzi wake kuwa umesajiliwa wapi na nani anaumiliki.

Aidha, elimu ya usalama wa usafiri wa vyombo vya majini ilitolewa kwa kuhimiza wavuvi, waendesha vyombo vya majini kuzingatia kutumia jaketi okozi kwa ajili ya usalama wao.Elimu hiyo ilitolewa katika mwalo wa Kimoyomoyo, Mrumo, Rulanda, Katunguru na maeneo mengine.

Sensa ya Vyombo Vidogo vya Uvuvi na Usafirishaji ni Sensa ya kwanza kufanyika nchini kupitia Shirika la Wakala wa Meli Tanzanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

0/Post a Comment/Comments