Watu
160 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo wakati wa Upimaji
ulioandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania
Na:
Mwandishi Maalum
Tarehe
30/09/2021. Watu 160 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo bila malipo wakati
wa upimaji ulioandaliwa na chama cha Madaktari Tanzania (MAT) uliofanyika
katika viwanja vya Hospitali ya Mkoa wa Geita na kumalizika jana.
Upimaji
huo wa siku tatu ulifanywa na wataalam wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
na kutoa rufaa kwa wagonjwa 14 Waliobainika kuwa na magonjwa mbalimbali ya
moyo.
Akizungumza
wakati wa upimaji huo Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophylly
Mushi alisema upimaji uliofanyika ni wa kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na
mabadiliko ya ndani ya muundo wa kuta za moyo unaosababishwa na shinikizo la
damu (Echocardioghraphy – ECHO), kuchunguza jinsi umeme wa moyo unavyofanya
kazi (Electrocardiography – ECG) pamoja na shinikizo la damu (BP).
“Kati
ya watu 160 tuliowaona, watu 118 (`73.5%) walikuwa na matatizo mbalimbali ya moyo,
watu 105 (65.6%) walikutwa na shinikizo la damu, watu 5 (3.1%) walikuwa na
shida ya valvu, watu 6 (3.7%) walikutwa kuta zao za moyo zikiwa zimetanuka (dilated
cardiomyopathy), watu 2 walikuwa na tundu kwenye moyo na watu 2 walihitaji
upasuaji mkubwa wa moyo kuziba matundu ya moyo”,
“Hata
hivyo walio kuwa na shida ya umeme wa moyo walikuwa watu 3, ambao kati yao
wawili wanahitaji kuwekewa betri ya moyo huduma inayotolewa katika taasisi yetu. Wagonjwa tuliowaona wengi wao hawakuwa wanajijua
kama wanamatatizo mbalimbali katika mioyo yao”, alisema Dkt. Mushi
Aidha
Dkt. Mushi alisema kuwa sambamba na upimaji huo, Taasisi ilitoa elimu ya afya ya
moyo, namna ya kuzuia magonjwa ya moyo pamoja na Lishe bora jambo ambalo lilifurahiwa
na wananchi wengi kwani elimu hiyo hawakuwahi kuipata.
Kwa
upande wake mwananchi aliyepata huduma katika banda la JKCI Zalphia Mzinga
amewashukuru wataalam wa JKCI kwa kugundua tatizo alilokua nalo kwa muda mrefu
kwani alikua akizimia mara kwa mara bila ya kujua kama anasumbuliwa na tatizo
la moyo.
“Nimekua
nikidondoka mara kwa mara bila kujua kama mapigo yangu ya moyo yapo chini, leo
hii nimefika katika banda la JKCI na kufanyiwa uchunguzi ambao ulionyesha
mapigo yangu yanapiga 28 kwa dakika nikapewa dawa, ushauri na kutakiwa kufika
Taasisi ya Moyo kwa ajili ya kuwekewa kifaa ambacho kitaongeza mapigo yangu ya
moyo”,
“Kwa
bahati mbaya wakati naendelea na huduma za matibabu katika mabanda mengine ile
hali ya kudondoka na kupoteza fahamu ikanitokea tana na kupata huduma ya
kwanza, sasa nimelazwa hapa Hospitali nasubiria rufaa ili niweze kupelekwa JKCI
kwa ajili ya kuwekewa pacemaker” alisema Zalphia
Naye
mwananchi kutoa mkoa wa Kagera Helena Christofa aliyetumia fursa ya kupata
huduma za matibabu baada ya kusikia kuwa kuna madaktari mabingwa wanatoa huduma
katika mkoa wa Geita, amewapongeza madaktari wa JKCI kwa kutumia muda mrefu kuwafanyia
wananchi uchunguzi wa kina ili kuweza kupata majibu yanayoridhisha.
“Kwakweli
nimekua nikienda hospitali kufanyiwa vipimo mbalimbali lakini sijawai ona
madaktari kama hawa wa JKCI wanaotumia muda wao mwingi kuhakikisha kuwa majibu
wanayoyatoa ni ya uhakika, nimeridhika na majibu niliyopewa, sasa naenda kuwa
balozi mzuri wa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza”,
Katika upimaji huo kampuni za uagizaji na usambazaji wa dawa za binadamu za Menarine, Kasmedics, SunPharma na Emcure zilitoa dawa bila malipo kwa wananchi waliokuta na matatizo ya moyo, kisukari na shinikizo la damu.
Post a Comment