ANDAENI PROGRAM ZA UKUZAJI AJIRA-MAJALIWA



............

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza wizara zote zenye dhamana ya ukuzaji ajira kuhakikisha zinaandaa programu na mikakati bora ya ukuzaji ajira ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wadau wote nchini washiriki katika utekelezaji wake ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezielekeza Ofisi na Wizara zote zenye dhamana za uwekezaji na biashara zihakikishe zinashirikiana na wadau wengine hususan sekta binafsi kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kutoa fursa ya kuanzishwa kwa viwanda vitakazochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira. 

ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Novemba 24, 2021) wakati akizindua Matokeo ya Viashiria Muhimu vya Soko la Ajira kutokana na utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2020/2021. Uzinduzi huo umefanyika katika Hotel ya Golden Tulip, Zanzibar.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa idadi ya watu walio na ajira nchini imeongezeka kutoka watu milioni 20.5 mwaka 2014 hadi kufikia watu milioni 24.1 mwaka 2020/2021, sawa na ongezeko la asilimia 17.5, ambapo kati yao wanaume ni milioni 12.4 na wanawake ni milioni 11.7.  

Aidha, amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa upande wake itahakikisha inaongeza kasi ya kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali zenye lengo la kuwezesha nguvukazi tuliyonayo kuajiriwa na kujiajiri.

Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuchambua viashiria vyote na kuhakikisha kuwa inakua na ripoti ya kina itakayowezesha maboresho mbalimbali ya kukuza ajira na uchumi nchini.

Amezipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na Ofisi ya Rais - Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar; Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar pamoja na wadau wa maendeleo kwa kufanikisha Utafiti huo.

Amesema lengo la utafiti huo ni kupata viashiria vya taarifa za soko la ajira ambavyo vitatumika kuwezesha Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo ya nchi yetu kupanga, kuhuisha na kufuatilia utekelezaji wa sera, programu na mikakati mbalimbali ya masuala ya ajira nchini.

“Utafiti huu unaviashiria vingi muhimu vinavyohusiana na masuala ya ajira nchini. Nitoe rai kwa wadau wote kupitia taarifa hii na kushirikiana na Serikali kuandaa na kutekeleza programu za pamoja za kukuza ajira kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuielekeza Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania ihakikishe inaweka utaratibu mzuri sambamba na kusimamia taasisi za fedha na mabenki nchini ili kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya biashara na uwekezaji.

 

0/Post a Comment/Comments