Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Malikale Bw Mwita William akifafanua jambo kwenye kikao cha Wizara ya Maliasili na Wadau wa Malikale wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Na Sixmund
Begashe
Serikali za mikoa ya Dar
es Salaam na Pwani zatakiwa kutambua kuwa urithi wa malikale uliopo
katika mikoa hiyo ni budi ulindwe na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa
na kijacho ili Malikale hizo ziendelee kutumika kama zao la utalii na, hivyo
kusaidia wananchi waliopo katika maeneo husika kujipatia kipato.
Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga kwa niaba ya Katibu Mkuu
wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Allan Kijazi kwenye kikao cha wadau wa
Malikale wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani ili kujadili ushiriki wa Serikali za
Mitaa na wadau katika uhifadhi na uendelezaji wa malikale.
Dkt Kijazi amesema kwa
kipindi cha hivi karibuni uhifadhi wa malikale katika nchi nyingi umeendelea
kuwa muhimu, kwani umeonekana kuvutia watalii wengi kutembelea maeneo ya
kihistoria, palentolojia na akiolojia. Kwa hapa nchini watalii wengi wamekuwa
wakitembelea Bonde la Olduvai na Mji Mkongwe wa Zanzibar.
”Katika Bara la
Afrika taarifa zinaonesha kuwa Nchi ya Siera Leone imefanikiwa kuendeleza njia
na maeneo yanayohusiana na utumwa kama vile mji wa kihistoria wa
Bunce ambao upo katika kisiwa cha Bunce kuwa kivutio cha utalii. Kisiwa
cha Bunce na mji wake ndilo eneo ambalo miaka 200 iliyopita, watumwa walikuwa
wakiondokea kutoka nchini Siera Leone kuelekea Bara la Amerika”. Aliongeza
Dkt Kijazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Chalinze Bw Ramadhani Possi licha ya kuipongeza Wizara kwa
kuwakutanisha wadau wa Malikale wa Mikoa ya Pwani, amesema kikao hicho kimekuwa
chachu kwao na kuahidi kuendelea kutenga fedha za kutosha ili zitumike
kuhakikisha uhifathi endelevu wa maeneo hayo unafanyika na kuvutia watalii
wengi kwenye Mbuga ya Sadani yenye historia kubwa.
Nae Afisa Utamaduni
Halmashauri ya Bagamoyo Bw Hamisi Kimenya, amesema kuwa Wilaya ya Bagamoyo
inautajiri mkubwa wa Malikale hivyo kupitia kikao hicho wao kama Afisa
Utamaduni wameongezewa wigo mpana wa uwelewa juu ya umuhimu wa uhifadhi wa
maeneo hayo na kuyaendeleza.
Mkurugenzi wa
Halmashauri Mkuranga Bi Mwantumu Mgonja nae licha ya kuipongeza Wizara ya
Maliasili kwa kikao hicho amesema Halmashauri yake imejipanga kikamilifu katika
kuhakikisha inaunga mkono jitihada za Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano Mama
Samiha Suluhu Hasan za kutangaza vivutio vya utalii ambavyo nipamoja na Malikale
ili viweze kuwanufaisha wananchi wa Kisarawe na Tanzania kwa Ujumala.
Katika kikao hicho Wizara ya Maliasili na Utalii nchini pamoja na wadau hao wa Malikale kutoka sekta ya Utamaduni na Kurugenzi za Halmashauri za Wilaya za Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamepata nafasi ya kujadili sera za uhifadhi na uendelezaji wa Malikale nchini.
Post a Comment