EPUKENI MITINDO YA MAISHA YEVYE ATHARI ZA AFYA -DKT. KIHOLONGWE*



Na.WAMJW,Dodoma


Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imeitaka jamii kuachana na mtindo usiofaa wa Maisha Ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Kauli hiyo  imetolewa Leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza  Dkt. James Kiholongwe wakati akitoa Elimu kwenye wiki ya kudhibiti magonjwa yasiyokuwa yakuambukiza ambapo amesema kuwa kuna kila sababu ya jamii kujizuia kuishi Maisha yanayoweza kuathiri afya.

Dkt. Kiholongwe amesema kuwa, watu wengi ambao wamekithiri katika matumizi ya pombe, uvutaji wa sigara, matumizi ya vyakula vyenye mafuta na kutokufanya mazoezi wamejikuta kwenye wimbi la kupata magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza hivyo kuathiri nguvu Kazi ya Taifa.

Dkt. Kiholongwe ameyataja baadhi ya magonjwa hayo kuwa ni pamoja na kisukari, ugonjwa wa Moyo, saratani, Figo na shinikizo la damu ambayo vichocheo vikubwa ni kuishi mtindo usiofaa wa Maisha usioendana na ulaji wa vyakula na vinywaji vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine Dkt. Kiholongwe ameitaka jamii kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi na kupima Afya mara kwa mara Ili kujua mwenendo wa afya kwani itasaidia kujiepusha na magonjwa hayo.

Wizara ya Afya inaadhimisha wiki ya Kitaifa ya kuzuia na kudhibiti  Magonjwa Yasiyoambukiza yenye kauli mbiu "Badili Mtindo wa Maisha,Boresha Afya" kuanzia tarehe  6 Hadi 13 Novemba kila mwaka na mwaka huu yanafanyika jijini Arusha na Mgeni Rasmi atakua Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima.
MWISHO

0/Post a Comment/Comments