Makumbusho ya Taifa nchini imeanza mchakato
wa ujenzi wa nyumba ya asili ya watu wa Zanzibar kama sehemu ya mkakati wake wa
kuendelea kuboresha mashirikiano katika uhifadhi wa urithi wa asili na utamaduni
na Idara ya Makumbusho na Malikale ya Zanzibar.
Akizungumza na wahifadhi kutoka
Zanzibar,Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa nchini,Dkt Noel Lwoga amesema
ni wakati sasa wa kuhakikisha Makumbusho ya Taifa kupitia Kijiji cha Makumbusho
iliyopo Kijitonyama Dar es Salaam, inabeba sura ya utanzania kwa kuwa na nyumba
ya asili ya Zanzibar.
Aidha Dkt Lwoga amesema kuwa nyumba hizo zimeanzia kwenye utafiti kutoka kwa wazee na wataalamu wa kihistoria lakini pia wamezingatia teknolojia iliyo bora.
Kwa upande wake Mhifadhi Mwandamizi wa Makumbusho ya Zanzibar, Kheri Bakari licha ya kuipongeza Makumbusho ya Taifa anaeleza namna walivyo lichukulia jambo hilo kuwa linaendelea kukuza utamaduni wa Zanzibar na hivyo kusaidia watalii kujifunza utamaduni wa Zanzibar.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kijiji cha Makumbusho Mawazo Ramadhani amesema ofisi yake pamoja na wataalam wamejipanga vyema kuhakikisha azma ya Taasisi kuwa na makazi hayo inafanyika mapema ili kutoa fursa ya watalii hasa wandani kujifunza na kuburudika kupitia uhifadhi huo wa kiutamaduni
Hata hivyo imeelezwa kuwa Dar es salaam itakuwa ni sehemu pekee ya wananchi na watalii kuweza kuona nyumba za utamaduni za mswahili lakini pia itakuwa ni alama ya kuelezea mtu anapotaka kwenda Zanzibar kuona uhalisia wake
Post a Comment