MABALOZI WA MAZINGIRA WATAKIWA KUSAIDIA KUDHIBITI UHARIBIFU WA MAZINGIRA



Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande akifungua warsha ya mazingira kuhusu utekelezaji wa kampeni  kabambe ya Hifadhi na usafi wa mazingira inayofanyika kwa siku mbili jijini Dar es salaam
Mabalozi na wadau mbalimbali wa mazingira nchini wakiwemo wabunge ambao wameshiriki katika warsha ya mazingira kuhusu utekelezaji wa kampeni  kabambe ya Hifadhi na usafi wa mazingira inayofanyika kwa siku mbili jijini Dar es salaam

.......................

NA MUSSA KHALID

Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Chande amewataka mabalozi wa mazingira nchini kuhakikisha wanasaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira ili vizazi vijavyo viweze kukuta nchi ikiwa na mazingira mazuri.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua warsha ambayo imewakutanisha mabalozi wa mazingira kuhusu utekelezaji wa kampeni  kabambe ya Hifadhi na usafi wa mazingira inayofanyika kwa siku mbili jijini Dar es salaam.

Naibu Waziri Chande amesema kuwa serikali imewaamini na kuwapa ubalozi ili kusaidia jamii kuweza kuishi kwa amani bila ya taharuki inayosababishwa na uharibifu wa mazingira.

‘Niwapongeze sana wataalamu wetu kwa kuwatafuta watu wakawaweka mabalozi kwani bila kujisimamia wenyewe hatotoka mtu nje ya nchi aje asimamie mazingira yetu bali tunayasimamia wenyewe’amesema Naibu waziri Chande

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Balozi wa Mazingira nchini Tanzania,Shekh Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhad Mussa Salum amewakumbusha watanzania kuwa utunzaji wa mazingira ni jambo la ibara kwani kufanya uharibu ni hatari kwa binadamu na viumbe wote.

Kwa upande wake Balozi wa Mazingira  na Kinara wa Umoja wa Mataifa katika malengo ya maendeleo endelevu Mwanamuziki Bernard Paulmaarufu kama Ben Pol ambaye Juni 6 mwaka huu aliteuliwa na Waziri Jaffo kuwa balozi wa mazingira amesema itawasaidia  kupambana na kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za uchafuzi wa mazingira.

Warsha hiyo imehudhuriwa na mabalozi na wadau mbalimbali wa mazingira nchini wakiwemo wabunge kwa lengo la kufanya uwasilisho kuhusu mpango kazi wa utekelezaji wa kampeni ya uhifadhi wa usafi wa mazingira.

0/Post a Comment/Comments