MADIWANI JIJI LA DAR WATAKA TARURA KUTOWALIPISHA USHURU WA MAEGESHO.


 Wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam wakisikiliza kwa makini katika kikao hicho.
Diwani mpya wa kata ya Buyuni ambaye ameapishwa hii leo katika kikao cha Baraza la madiwani jiji la Dar es salaam

Meneja wa TARURA Ilala Samweli Ndoveni akitolea ufafanuzi kuhusu madiwani kutozwa ushuru wa maegesho
............................

NA MUSSA KHALID,DAR ES SALAAM

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam limeitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini  (TARURA) kupitia muongozo na kuangalia namna ya kutowalipisha madiwani ushuru wa maegesho kwani wao ndio wanaidhinisha fedha za wao kutengeneza barabara.

Hayo yamejiri leo jijini Dar es salaam katika kikao cha Baraza la Madiwani wa jiji hilo ambacho kimeongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji na Mwenyekiti wa baraza hilo Omary Kumbilamoto wakati wakijadili taarifa za utekelezaji kamati mbalimbali kuanzia kipindi cha Julai mpaka Septemba mwaka huu sambamba na kumuapisha Diwani mpya wa kata ya Buyuni.

Madiwani hao wamesema wanakumbana na changamoto pindi wanapoegesha vyombo vya vyao vya usafiri kwa kulipishwa ushuru hivyo wameeleza kuwa ni vyema TARURA ikawafutia tozo hizo kutokana na kuwa wao wanawahudumia wananchi.

Akijibu maazimio ya wajumbe hao wa baraza la madiwani kuhusu msamaha wa ushuru wa maegesho,Meneja wa TARURA Ilala Samweli Ndoveni amesema atahakikisha analishughulikia suala hilo ili liweze kupatikana ufumbuzi.

Kuhusu suala la ujenzi wa barabara Mstahiki Meya wa jiji la Dar es salaam Kumbilamoto amesema wamekubaliana na TARURA ndani ya mwezi mmoja madiwani wafanye mapitio ya taarifa ya maeneo yao ili kuanza uboreshaji barabara hizo.

Katika Hatua nyingine imeelezwa kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam imekusanya takriban Tsh.Bill 17.7 sawa na asilimia 95 katika kipindi cha robo ya kwanza kuanzia mwezi Julai mpaka septemba mwaka huu kutoka katika vyanzo vya ndani na ruzuku serikalini.

0/Post a Comment/Comments