MFUMO WA KIELEKTONIKI WA MALIPO YA MAEGESHO KUANZA TAR 1 DISEMBA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu

Serikali imesema kuwa mfumo wa Kieletroniki wa malipo ya ada ya maegesho utaanza tena kutumika Desemba Mosi 2021 baada ya kujitokeza changamoto mbalimbali katika mfumo wa awali uliosimikwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amesema Oktoba 9, 2021 alisitisha kwa muda matumizi ya mfumo wa zamani wa TARURA baada ya kuwepo malalamiko kwa Wananchi waliokuwa wanatumia Mfumo huo husika hususani maeneo ya Dar es Salaam.

Waziri Ummy amesema mfumo huo mpya ulioundwa na TARURA umeboreshwa kwa kiasi kikubwa ili kuondoa kero na changamoto za awali zilizojitokeza kwa Watumiaji ikiwemo changamoto ya Wananchi hao kufungiwa Minyororo kwenye Magari yao, kuokoa muda katika kulipa ushuru wa maegesho, Ukwepaji kulipa Kodi na kurahisisha ukusanyaji wa ushuru.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amesema TARURA wanahusika zaidi kwenye eneo la Hifadhi za Barabara zilizo chini ya Wakala huo, amesema nje ya hapo hawahusiki na usimamizi wa ukusanyaji wa malipo ya ushuru.

Kuhusu suala la kutotoa risiti, Mhandisi Seff ameeleza kuwa suala hilo watalifuatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha Risiti zinatolewa kwa Watumiaji wa maeneo hayo ya maegesho pale watakapolipa ada.


Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Geofrey Mkinga amesema tangu kuanza kuutumia mfumuo huo umesaidia kuongezeka kwa ukusanyaji wa malipo lakini pia umedhibiti mianya ya upotevu wa makusanyo.

 

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema serikali imepunguza faini ya kupitiliza muda wa malipo ya maegesho kutoka Sh30,000 hadi Sh10,000 huku muda wa malipo ukiongezwa kutoka Siku 7 hadi 14.


0/Post a Comment/Comments