Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua mfumo unganishi
wa taarifa za ardhi katika ofisi ya ardhi Manispaa ya Ubungo mkoa wa Dar
es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua uendaji kazi wa sekta ya ardhi.
Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na watendaji wa
sekta ya ardhi pamoja na Wawakilishi wa Makampuni ya DIMWE Conslt Ltd na MOSAIK
Company Ltd kwenye ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dar es Salaam
wakijiridhisha kupitia mfumo madai ya baadhi ya Kampuni kuwa watendaji wa ardhi
wanachelewesha kazi za Makampuni hayo katika zoezi la Urasimishaji.
................
Na Munir
Shemweta, WANMM
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikitishwa na baadhi
ya Makampuni yanayofanya kazi za urasimishaji makazi holela mkoa wa Dar es
salaam kutuhumu watendaji wa sekta ya ardhi kuwa wanachelewesha kazi
wakati tatizo liko ndani ya makampuni yao.
Katika kikao chake na
watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya Manispaa ya ubungo pamoja na
makampuni yanayofanya kazi ya urasimishaji makazi holela kwenye manispaa hiyo,
makampuni hayo yalimueleza Naibu Waziri Dkt Mabula kuwa yanashindwa kukamilisha
kazi kwa wakati kutokana na watendaji wa sekta ya ardhi kushindwa kutoa kazi za
upimaji wanazopeleka ofisi za ardhi kwa wakati.
Kufuatia tuhuma hizo
Dkt Mabula aliyataka makampuni hayo kufika ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi
mkoa wa Dar es Salaam kuangalia mfumo wa miamala ya ardhi kwa lengo la kubaini
wanaokwamisha kazi ili aweze kuchukua hatua.
Hata hivyo, wakati wa
kupitia kazi za makampuni kwenye mfumo Novemba 4, 2021 ilibainika kuwepo uzembe
kwa baadhi ya makampuni kwa kushindwa kufuatilia kazi zao ama kutokuwa na
mawasiliano watu wanaowatuma kufuatilia kazi zilizopelekwa Wizarani.
‘’Mfumo wa sasa hivi
haudanganyi kabisa na ardhi ya sasa siyo ile ya zamani hata mtu akifanya vurugu
ama kutegea kufanya kazi atagundulika tu kwa kuwa kila kitu kiko katika mfumo,
ninyi taarifa mmepewa tangu mwezi wa sita halafu mnailaumu wizara’ alisema Dkt
Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwaeleza wawakilishi wa makampuni DIMWE Land
Consult Ltd na MOSAIK Company Ltd yaliyofika ofisini kwa Kamishna kuwa,
sasa hivi ukitaka kufuatilia kazi za ardhi kupitia mfumo kuanzia mwanzo hadi
mwisho utaipata na utagundia uzembe uko kwa mtendaji gani na kusisitiza kuwa,
kwa sasa hakuna tena udanganyifu kama ilivyokuwa ikifanyika zamani.
Awali katika ziara
yake Naibu Waziri Dkt Mabula alikagua mfumo Unganishi wa Taarifa za ardhi
katika ofisi ya ardhi Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam na kujionea utendaji
kazi pamoja na changamoto zinazowakibili watendaji wa sekta ya ardhi ambapo
akiwa katika ofisi hiyo aliwataka watendaji hao kuongeza kasi ya utoaji hati za
ardhi.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi alizungumza na wakazi wa Mbezi kwa Yusufu kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili kuhusiana na sekta ya ardhi sambamba na kutoa hati kwa wananchi waliorasimishiwa makazi yao ambapo hata hivyo, wengi wa wananchi katika mkutano huo walilalamikia makampuni ya urasimishaji makazi holela kwa kuchelewesha kazi huku makampuni hayo yakiwa yamechukua fedha za wananchi.
Post a Comment