Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia sehemu ya
Jengo la Kibiashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo Mutukula
wilayani Misenyi mkoani Kagera alipokwenda kukagua mradi wa jengo hilo.
Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo
kutoka kwa Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera Maneno Mahenge
(Kulia) alipokwenda kukagua Jengo la Kibiashara la Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC) katika eneo la Mutukula wilayani Misenyi mkoani Kagera
Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifurahia bidhaa
aliyonunua kwenye moja ya maduka yaliyopanga katika jengo la Kibiashara la
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo Mutukula wilayani Misenyi
mkoani Kagera alipokwenda kukagua mradi wa jengo hilo.
.....................................
Na Munir Shemweta, MISENYI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amelitaka Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) kuendelea kuwekeza miradi ya kimkakati itakayoliwezesha shirika
kujiongezea kipato.
Dkt Mabula ametoa kauli hiyo tarehe 23 Novemba 2021 wakati akikagua mradi wa
jengo la kibiashara la NHC lilipo mpakani mwa Tanzania na Uganda eneo la Mutukula
wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.
Naibu Waziri ambaye alikuwa katika ziara ya siku mbili mkoani Kagera
alisema, ilichofanya NHC kujenga jengo la kibiashara katika mpaka wa Tanzania
na Uganda Mutukula ndicho serikali inachokitaka pale inapokuwa na taasisi
zinazojitegemea katika uendeshaji pia ziwe na njia tofauti za kujiongezea
kipato kitakachosaidia kuongeza miradi mingine.
" Hiki ambacho NHC mmekifanya hapa kujenga jengo la biashara Mutukula
ndicho inachokitaka serikali kuwa inapokuwa na taasisi inayojitegemea
kiuendeshaji pia iwe na njia tofauti za kujiongezea kipato cha shirika "
alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Dkt Mabuka, mradi wa jengo la biashara Mutukula unatoa fursa kwa
wafanyabiashra kutoka nchi jirani ya Uganda kuja Tanzania kununua bidhaa kwani
awali ilikuwa aibu kuona wafanyabiashara wakienda kununua bidhaa katika maduka
ya nchi hiyo.
" Ilikuwa aibu tunaenda upande wa pili kununua bidhaa lakini sasa na wao
waje hapa kufanya biashara na hii ni alama tosha kuwa tunaanza kubadilika"
alisema Naibu Waziri Mabula.
Aidha, Dkt Mabula aliongeza kuwa, ana imani mradi wa jengo la kibiashara
Mutukula ukienda vizuri eneo lingine linalokusudiwa kujenga maduka litapata
msaada wa fedha za ndani zitakazopatikana kupitia mradi huo.
Naibu Waziri Mabula aliongeza kuwa, ni kweli wafanyabiashara wadogo
wamachinga hawawezi kupanga katika jengo la mradi huo lakini shirika linaweza
kujenga maduka kuzunguka jengo hilo yanayoweza kubadilisha sura ya eneo
kuonesha kuwa eneo hilo limepangwa na isiwe viduka visivyoonesha tofauti kati
ya eneo lilipangwa na lisilopangwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Projestus
Tegamaisho Mutukula amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa uamuzi wake wa
kuwekeza mradi huo katika eneo la Mutukula ambapo aliiomba NHC kuangalia
uwezekano wa kuwekeza mradi kama huo katika mji unaopanuka wa Bunazi wilayani
Misenyi.
"Niwashukuru NHC kwa kutuwekea kitega uchumi cha jengo hili na tunaomba
mtujengee jengo lingine katika mji wa Bunazi ili maeneo ya Misenyi yawe na
uwelezaji mkubwa" alisema Tegamaisho.
Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera Maneno Mahenge alisema,
mradi wa jengo la Mutukula kwa sasa umefikia asilimia 99 na mradi huo umetumia
asilimia 50 tu ya eneo lake lenye ukubwa wa mita za mraba 7900.
" Tunataka mradi huu wa kitega uchumi hapa Mutukula uwe shopping centre
area inayotembelewa na wananchi wengi wakiwemo wa nchi jirani ya Uganda na
jengo hili tayari lina wapangaji 36" alisema Mahenge.
Aidha, katika kuhakikisha NHC unawekeza majengo ya kimkakati maeneo ya mipakani
Meneja huyo wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera alieleza kuwa, tayari
amepeleka Andiko Makao Makuu ya NHC kwa ajili ya kuanzisha miradi kama wa
Mutukula katika eneo la Rusumo mpaka wa Tanzania na Rwanda pamoja na Kabanga
katika mpaka wa Tanzania na Burundi.
Post a Comment