Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 2 Novemba, 2021, amehutubia
mkutano wa Wakuu wa nchi wanaoshiriki mkutano wa 26 kuhusu mabadiliko ya
tabianchi na kutoa wito kwa mataifa yote kuwa juhudi za pamoja zinahitajika kwa
kuwa athari za mabadiliko hayo hazichagui nchi zilizoendelea au zinazoendelea.
Mhe. Rais Samia ameeleza namna
mabadiliko ya tabianchi yanavyoiathiri Tanzania katika ardhi ya uzalishaji
mali, ongezeko la kina cha bahari, kuyeyuka kwa barafu katika kilele cha Mlima
Kilimanjaro, namna ambavyo kisiwa cha
Zanzibar kinavyoathirika kwa ongezeko la kiwango cha joto ambalo linaathiri
ekolojia inayovutia watalii.
Aidha, ameongeza kuwa athari hizo
zinatokea licha ya Serikali ya Tanzania kuendelea na azma yake ya kutenga hekta
milioni 48 kwa ajili ya utunzaji wa misitu.
Mhe. Rais Samia ameeleza pia kuwa
Serikali ya Tanzania inao mkakati maalum wa kupambana na mabadiliko ya
tabianchi ambao umeainisha hatua kadhaa za kuchukua ikiwemo kupunguza athari za
hewa ukaa kwa asilimia kati ya 30 na 35 ifikapo mwaka 2030.
Mhe. Rais Samia amehimiza nchi
zilizoendelea kutimiza ahadi zao za kuratibu upatikanaji wa kiasi cha Dola za
kimarekani bilioni 100 kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi
hususan kwa nchi zinazoendelea kwa kueleza kuwa athari zikitokea zitawakumba
wote, nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Wakati huo
huo,
Mhe. Rais Samia pia ameshiriki na kuzungumza katika mkutano maalum wa viongozi
wanawake wanaoshiriki Mkutano wa 26 wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa
kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi (COP26) ulioitishwa na Kiongozi wa
Serikali ya Scotland, Bi. Nicola Sturgeon.
Mhe. Rais Samia ameelezea namna
wanawake duniani na hususan Tanzania wanavyoathirika na mabadiliko ya tabianchi
na kutoa wito kwa hatua madhubuti kuchukuliwa ili kuwasaidia wanawake na jamii
nzima kwa ujumla. Pia ametoa wito wa kushirikisha wanawake katika utungaji wa
sera za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Mhe. Rais Samia pia ameeleza
namna Tanzania ilivyo mstari wa mbele katika kushirikisha wanawake kwenye
mapambano ya mabadiliko ya tabianchi na kusema kuwa Tanzania ina mkakati maalumu
wa Kitaifa wa Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi tangu mwaka 2013 ambao umekuwa
na lengo la kuhakikisha wanawake wameshirikishwa kikamilifu katika eneo la
mabadiliko ya tabianchi.
Mara baada ya Mkutano huo, Mhe. Rais
Samia pamoja na viongozi wengine Wanawake waliohudhuria mkutano huo wamesaini
tamko la pamoja kuhusu kupaza sauti katika kukabiliana na athari za mabadiliko
ya tabianchi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Post a Comment