........................
Na Abubakar W Kafumba, UAE
Novemba 12 Mwaka huu ujumbe kutoka banda la Tanzania ukiongozwa na Mkurugenzi wa Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai, Bi. Getrude Ng'wesheni kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) aliyeambatana na wawakilishi wa Taasisi zinazoshiriki zikiwemo Shirika la Uwekezaji (TIC) na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi la Ngorongoro (NCAA) wametembelea Banda la Eswatini.
Ujumbe huo ulipokelewa na Mkurugenzi wa Banda la Eswatini Bi. Chunky Mdluli na mwakilishi kutoka Mamlaka ya Utalii ya Eswatini Bi. Zotheni Mabusela.
Tanzania na Eswatini zikiwa ni miongoni mwa mataifa 54 ambayo ni sehemu ya Umoja wa Afrika (AU) kwa pamoja zimeona kuna haja ya kuja pamoja ili kuleta maendeleo endelevu ya pamoja kwa kushirikiana kupitia sekta mbalimbali.
Kati ya mambo yalioongelewa katika kikao hicho ni fursa za uwekezaji na maeneo ambayo Tanzania na Eswatini wanaweza kushirikiana. Vipaumbele vikuu vimewekwa katika sekta za Utalii, Kilimo, Ufugaji, Elimu na Afya.
Mkurugenzi wa Banda la Eswatini Bi. Chunky Mdluli ameeleza kuwa Eswatini ipo tayari kushirikiana na Tanzania na inatarajia kufanya kikao kingine ambapo kwa pamoja na wataweka mipango ya utekelezaji wa namna mzuri ya kushirikiana ili kuweza kutumia fursa ya kushiriki kwenye maonesho haya ya Dunia ya Expo 2020 Dubai kuleta maendeleo ya kisekta baina ya Tanzania na Eswatini.
Post a Comment