Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania Veeraya Kate Somvongsiri (Kulia) akizungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alipokwenda kukutana na Waziri wa Ardhi William Lukuvi ofisini kwake eneo la Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma tarehe 11 Novemba 2021.
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania
Veeraya Kate Somvongsiri (wa pili kushoto) na viongozi wa Wizara alipotembelewa
na Mkurugenzi huyo wa USAID ofisini kwake eneo la Mji wa Serikali Mtumba mkoani
Dodoma tarehe 11 Novemba 2021.
........................
Na Munir
Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekutana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika
la Maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania Veeraya Kate Somvongsiri na
kumuelezea hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha sekta ya ardhi
nchini.
Bi Kate alimtembelea
Waziri Lukuvi katika Ofisi za Wizara zilizopo eneo la Mji wa Serikali Mtumba
mkoani Dodoma leo tarehe 11 Novemba 2021 kwa lengo la kujitambulisha.
Katika mazungumzo yao,
Waziri Ardhi alimueleza Mkurugenzi huyo wa USAID nchini kuwa, Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko katika jitihada mbalimbali kuhakikisha ardhi
yote ya Tanzania inapangwa na kupimwa.
Kwa mujibu wa Lukuvi,
pamoja na juhudi hizo, Wizara yake imeanza pia kuhifadhi kumbukumbu za ardhi
kwa kutumia mfumo wa kidigitali na kuachana na ile mifumo ya zamani iliyokuwa
ikitumia karatasi nyingi huku ikianza kutoa hati za ardhi za kielektroniki
yenye kurasa moja.
‘’Tunataka kwenda
mbele zaidi katika teknolojia ya uhifadhi wa kumbukumbu zetu za ardhi na
tumeanza kuscan taarifa zetu za ardhi katika teknolojia na tumeanza pia kutoa
hati za kielektroniki kwenye mkoa wa Dar es salaam na Dodoma’’ alisema Lukuvi.
Naye Katibu Mkuu
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema, pamoja
juhudi za Wizara kuhakikisha ardhi inapimwa vipaumbele pia vimeelekezwa kwenye
maeneo ya vijijini ikiwemo kutumia njia rahisi ya upimaji na kutoa hati za
kimila ili kulinda maeneo pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
‘’Kwa sasa wizara ya
ardhi inafanya jitihada kubwa kuhakikisha ardhi inapangwa na kupimwa ili
kuepuka migogoro ya ardhi na wakati huo kuwawezesha wananchi kiuchumi pamoja na
kuiwezesha serikali kupata mapato.’’ Alisema Mary
Kwa Upande wake
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani USAID Veeraya Kate
Somvongsiri aliunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kupitia Wizara ya
Ardhi na kusema kuwa Shirika hilo liko tayari kushirikiana na wizara ya ardhi
kusaidia sekta ya ardhi nchini.
‘’Nimetembelea mkoa wa
Iringa kunakofanyika mradi wa upimaji ardhi wa teknolojia rahisi vijijini (Feed
the Future Tanzania Land Tenure Assistance) na kuona jinsi mradi huo
ulivyofanikiwa ambapo niliangalia namna bora ya kusaidia miradi kama hiyo na
nimeomba kupatiwa proposal kuhusiana na mafanikio ya mradi’’.alisema Kate
Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Maendeleo la Marekani USAID imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali nchini Tanzania katika nyanja za nishati, uhifadhi wa mazingira, huduma za afya ya uzazi na afya ya mtoto, huduma za kubabiliana na malaria na msaada kwa wakimbizi.
Post a Comment