Rais Samia Suluhu Hassan, ahutubia katika hafla ya uwekaji saini Makubaliano kati ya Serikali na Kampuni 4 za Uchimbaji Madini nchini, iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Convention Centre Jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Desemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akishuhudia makabidhiano ya Hati mara baada ya tukio hilo la kusaini makubaliano kati ya Serikali na Kampuni za uchimbaji Madini za Black Rock Mining Limited, Strandline Resources Limited na Nyanzaga katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Convention Centre Jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Desemba 2021. PICHA NA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akishuhudia tukio la Utiaji Saini makubaliano kati ya Serikali na Kampuni za Uchimbaji Madini za Black Rock Mining Limited, Strandline Resources Limited na Nyanzaga katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Convention Centre Jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Desemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza kwenye hafla ya utiaji Saini makubaliano kati ya Serikali na Kampuni 4 za Uchimbaji wa Madini za Black Rock Mining Limited, Strandline Resources Limited na Nyanzaga katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Convention Centre Jijini Dar es Salaam leo tarehe 13 Desemba 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Madini na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuongeza nguvu katika kudhibiti wizi na utoroshaji wa madini hasa katika maeneo ya bandari, viwanja vya ndege na mipakani ili kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zinaleta manufaa kwa taifa.
Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa Serikali iliamua kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria zinazosimamia sekta ya madini ili kuipa nguvu Serikali kumiliki rasilimali hizo kwa niaba ya wananchi kwa nia ya kuleta manufaa zaidi kwa watanzania.
Vile vile, Mhe. Rais Samia amesema kutokana na maboresho yaliyofanywa katika sekta ya madini, anatarajia mchango wa sekta hiyo kufikia asilimia 10 kwenye pato la taifa hadi kufikia mwaka 2025.
Mhe. Rais Samia amesema kampuni hizo za ubia ndizo zitakazosimamia uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali yaliyotolewa leseni za uchimbaji ili kuhakikisha maslahi ya nchi yanasimamiwa ipasavyo.
Pia, Mhe. Rais Samia amesema kupitia miradi hiyo, Serikali itapata manufaa mbalimbali ikiwemo kodi, tozo, ajira, huduma kwa jamii, ununuzi wa bidhaa na huduma zinazopatikana hapa nchini.
Mhe. Rais Samia pia ameitaka Wizara ya Madini isimamie kikamilifu suala la uongezaji thamani ya Madini nchini na kubainisha kuwa uchenjuaji wa madini utafanyika Tanzania na sio nchi nyingine.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesisitiza kuwa madini yetu yatachimbwa, kuchenjuliwa na kuongezwa thamani hapa nchini ili kuweza kupata faida tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali.
Kampuni hizo zinatarajiwa kuwekeza shilingi Trilioni 1.75, ambapo miradi hiyo pamoja na kuipatia mapato Serikali pia itatoa fursa za ajira, gawio na biashara kupitia huduma zitakazotolewa katika maeneo ya uchimbaji, uchenjuaji na usafirishaji wa madini yatakayozalishwa.
Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa viongozi wa Serikali kuwashirikisha wananchi wakati wa kupanga utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuwapatia elimu ili waweze kuelewa umuhimu wake na kuondoka migogoro isiyo kuwa na ulazima.
Mhe. Rais Samia amewataka wawekezaji kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia sekta hiyo na kuagiza Baraza la Mazingira nchini (NEMC), Serikali za Mitaa pamoja na wawekezaji kusimamia utunzwaji wa mazingira kama Sheria ya Mazingira inavyobainisha na kuhakikisha kuwa miradi hiyo haileti athari katika maeneo mbalimbali.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia ameshuhudia utiaji Saini ya Makubaliano kati ya Serikali na Kampuni ya Nyanzaga Mining Ltd itakayochimba madini ya Dhahabu Jijini Mwanza, Kampuni ya Petra Diamond Ltd inayoendelea na uchimbaji madini ya Almasi Mkoani Shinyanga, Kampuni ya Black Rock Mining Ltd (Mahenge Resources) itakayochimba madini ya Kinywe (Graphite) Mkoani Morogoro na Kampuni ya Strandline Resources Ltd itakayochimba madini ya Heavy Mineral Sand katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi `wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Post a Comment