Naibu Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini zamani Swaziland na Mkewe Bi Dimpho Masuku wakitazama sanamu zinazoelezea biashara ya Utumwa, Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Jijini Ilala Dar es Salaam
...................................
Na Sixmund J. Begashe
Naibu Waziri Mkuu wa Ufalme wa
Eswatini zamani Swaziland, alieambatana na Mkewe Bi Dimpho Masuku na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe Thulisile Dlodla wameitembelea
Makumbusho ya Taifa ili kujionea uhifadhi adhimu wa historia ya nchi na urithi
wa asili na utamaduni uliohifadhiwa na kuoneshwa Makumbusho na Nyumba ya
Utamadani Dar es Salaam.
Mhe Masuku alipokelewa na Mkurugenzi
Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga, Mkurugenzi wa Makumbusho na
Nyumba ya Utamaduni Bw Achiles Bufure kisha kutembezwa kwenye kumbi mbalimbali
zilizo beba Historia ya nchi, Chimbuko la Mwanadamu, Sanaa, michoro ya
mapangoni, Bustani ya Vipepeo, na Maktaba ya kihistoria.
Akiwa Makumbusho na Nyumba ya
Utamaduni Mhe. Masuku na mkewe walipata nafasi pia ya kuingia chumba mahususi
ambako walijionea fuvu la binadamu wa kale Zinjanthropus anaesadikiwa kuishi
miaka milioni 1.7 iliyo pita, hati ya Uhuru, tai zilizovaliwa siku ya Uhuru,
vifaa vilivyotumika kuchanganyia udongo wa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar
nk.
Baada ya ziara hiyo Mhe Masuku
aliipongeza Makumbusho ya Taifa kwa hatua kubwa iliyo piga katika uhifadhi wa
urithi wa Utamaduni na wa Malikale, huku akimwagiza Waziri wa Mambo ya Nje wa
nchi hiyo, Mhe Thulisile Dlodla kuhakikisha ofisi yake inaipatia Makumbusho ya
Taifa taarifa na nyaraka muhimu zinazo husu usafirishwaji wa watumwa kwenye
Miji ya Lusaka, Nairobi na Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya
Taifa Dkt Noel Lwoga amemshukuru Mhe Masuku na Ujumbe wake kwa kuona umuhimu wa
kuitembelea Makumbusho ya Taifa ili kujifunza na kujionea uhifadhi wa urithi
adimu na adhimu unao husu utamaduni na malikale za Tanzania, Afrika na dunia
kwa ujumla.
Sanjari na pongezi hizo, Dkt Lwoga
alimpatia Mhe Masuku zawadi ya vitabu vya historia pamoja na Vikombe vyenye
kauli mbiu za program zinazoendeshwa na Taasisi yake.
Naibu Waziri Mkuu huyo Mhe Masuku yupo hapa nchini kumwakilisha Mfalme Mswati wa Tatu katika maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania yanayo tarajiwa kuadhimishwa kitaifa Desemba 9 Mkoani Dar es Salaam ambapo Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani atakuwa mgeni Rasmi.
Post a Comment