TET YAKUTANA DODOMA KUPEANA UZOEFU WA UBORESHAJI WA MITAALA

 



Na Mwandishi Wetu, Dodoma. 

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeiagiza  Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuhakikisha wataalamu wake wanapata nafasi ya kujifunza uzoefu  kutoka nchi nyingine utakaowawezesha  katika kufanya maboresho ya mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ualimu.


Hayo yamesemwa na Kaimu Kamishna wa Elimu nchini, Bwana Venance  Manori ambaye amemwakilisha   Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo katika mkutano wa kupeana uzoefu katika uboreshaji wa mitaala unaofanyika Mkoani Dodoma katika ukumbi wa  Hazina kuanzia tarehe 8 hadi  9/12/2021.


Amesema majadiliano ya uzoefu wa kuboresha mitaala kwa nchi nyingine yatawezesha wataalamu wa  hapa nchini kufanya kazi hiyo kwa weledi.


“Naamini mtatumia  fursa hii adhimu ya uzoefu wa nchi nyingine  kwa ajili ya kupata ujuzi wa kuendelea na kazi ya maboresho ya mitaala iliyoanza hapa nchini," amesema Akwilapo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt.Aneth Komba  amesema mkutano huu una lengo la kuwajengea uzoefu wakuza mitaala juu ya namna nzuri ya kufanya  kazi ya mapitio ya mitaala.


“Kazi ya maboresho inaendelea kwa sasa iko katika hatua ya kupata maoni kwa wadau mbalimbali nchini, hivyo uzoefu wa nchi nyingine utatuwezesha kupata uelewa mpana katika kazi hii ya maboresho ya  mitaala," amesema Dkt. Aneth


Kwa upande wake Mkurugunzi Msaidizi Sekondari, kutoka Wizara Ofisi ya Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI), Bi Khadija Mcheka amesema, majadaliano hayo ya kupata uzoefu wa kuboresha mitaala kwa  nchi nyingine yatasaidia sana katika kupata elimu iliyo bora nchini hasa katika zoezi la uboreshaji mitaala linaloendelea.


TET imefanikiwa kupata uzoefu wa uboreshaji mitaala ya elimu kutoka nchini Kenya ambayo ilitumia muda wa miaka mitano katika kufanya maboresho yao,ambapo  kwa Tanzania  zoezi la uboreshaji Mitaala linatarajiwa kutumia miaka minne na mitaaala mipya kuanza kutumika mwaka 2025.






0/Post a Comment/Comments