MIKOA 17 TANZANIA BARA NA VISIWANI YAKABISHIWA VIFAA VYA KUJIKINGA NA UVIKO -19 VYENYE THAMANI YA MILIONI 57



Mratibu wa kitaifa programu ya kuzuia na kukabiliana na Upungufu wa Vitamini A nchini kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Francis Modaha(Kulia),akimkabidhi Mganga mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Aifillo Sichalwe Chupa ya Kitakasa Mikono ikiwa ni ishara ya kumkabidhi vifaa vya  kupambana na UVIKO-19.


        ***************************



Na Asha Mwakyonde,Dodoma


WIZARA  ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhi vifaa vya kujikinga na UVIKO-19 Mikoa 12 ya Tanzania Bara na 5 ya Zanzibar lengo likiwa ni kuwakinga watoa huduma za afya hasa katika utoaji wa matone ya Vitamini A nchini.


Vifaa hivyo vimetolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC),kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI), kwa lengo la kuwakinga watoa huduma hao ambavyo ni  Katoni 6000 za Barakoa (Mask) na Vitakasa Mikono (Sanitizer) lita 6000 vyenye gharama ya Milioni 57.


Akizungumza jijini Dodoma leo Januari 5, 2022 wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa wawakilishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira Mganga Mkuu wa Serikali Dk.Aifillo Sichalwe amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya na wale  watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW).


Ameitaja mikoa 12 ya Tanzania Bara ambayo imepata vifaa hivyo kuwa ni Dodoma,Kagera,Mwanza,Geita, Morogoro, Kilimanjaro, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Singida,Tanga na Katavi  na ile mitano ya Zanzibar.


Dk.Sichalwe amefafanua kwamba mikoa mitano ya Tanzania Visiwani imeteuliwa kwa kuwa ilikuwa na ufanisi duni kwenye  utoaji wa huduma za mwezi wa afya na msaada huo utasaidia kuimarisha kiwango cha utoaji wa huduma za matone ya Vitamini A kwa watoto wengi zaidi nchini.


"Serikali inaendelea kuwapatia vifaa hivi ili  kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 kwa watoa huduma waliopo  vituo vya  afya  lengo likiwa ni  kuendelea kutoa huduma hizi  kwa ufanisi  pamoja na  Kampeni ya utoaji wa Matone ya Vitamini A ambayo inafahimika kama Huduma ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto," amesema.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dk. Ray Masumo 

ameeleza kuwa vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za  afya waliopo mstari wa mbele katika kutoa hudama hizo  pamoja na ile ya  Huduma ya mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto kwa kuwa  malengo yake ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 watoto wote nchini wanafikiwa na huduma ya matone ya Vitamini A kupitia vituo vya afya vilivyopo nchini.


"Naishukuru Serikali ya Cananda kupitia Shirika lake la Nutrition International kwa kuendelea kuiunga mkono serikali yetu katika  vita dhidi ya UVIKO-19 pamoja na changamoto nyingine za Kilishe," amesema Dk Masumo.


Naye  Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI) Dk.Daniel Nyagawa amesema wametoa vifaa hivyo  kwa Serikali ya Tanzania  lengo likiwa ni  kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali  kwenye kupambana na  UVIKO-19.


"Tutaendelea kushirikiana katika masuala mbali mbali yakiwemo ya Kilishe ambapo shirika hili limekuwa likiyatekeleza hapa Tanzania," amesema.


Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mkurugenzi wa huduma za Afya Dk.Mwanahamisi Hassan amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya waliopo mstari mbele katika vita ya UVIKO-19.


Aidha anawakaribisha wadau wengine kujitokeza  katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali katika vita ya kujikinga na UVIKO-19.



Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Aifillo Sichalwe (Kulia), akikabidhi Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mohamed Abdulla  boksi la kitakasa mmkono kwa ajili ya Mikoa 5 ya Zanzibar ikiwa ni  ikiwa ni ishara ya kupokea vifaa vya kuwakinga na UVIKO-19 watoa huduma za afya wakati wa huduma za Mwezi wa afya na Lishe ya Watoto.




Mkurugenzi wa huduma za Afya- TAMISEMI Mwanahamisi Hassan (Kulia), akimkabidhi kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Samuel Seseja boksi la Barakoa ikiwa ni ishara ya kupokea vifaa vya kuwakinga na UVIKO-19 kwa niaba ya Wganga Wakuu wa Mikoa 12 nchini, ambayo itapatiwa vifaa hivyo.

MWISHO

0/Post a Comment/Comments