Na Mwandishi Wetu
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga kimeibuka na kumuombea radhi Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai kwa Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia hotuba yake aliyotoa hivi karibuni iliyodaiwa kuwa imemvunja moyo Rais.
Chama hicho kimesema Spika Ndugai kama walivyowanachama wengine alikengeuka na kukosea lakini ametambua makosa yake na kuomba msamaha hivyo wanamuombea radhi kwa Rais.
Hata hivyo tayari Spika Ndugai amemuomba radhi Rais Samia na kusema kuwa hotuba yake haikuwa na jambo la kukashifu wala kudharau juhudi za Serikali bali alikuwa anasisitiza ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa amesema hakuna mtikisiko wowote utakaotokea ndani ya CCM na kusisitiza kuwa Ndugai kama binadamu wengine alipotoka na kukengeuka ila ametambua makosa na kuomba radhi.
"Kama walivyowanachama wengine waliwahi kukengeuka na kukosea lakini waliomba radhi hadharani hivyo kwa niaba ya wanaCCM mkoa wa Shinyanga namuombea radhi Ndugai kwa Rais Samia kutokana na makosa aliyoyafanya ambayo amekiri mwenyewe kuwa amekosea," amesema
Hata hivyo amesema kitendo cha Spika Ndugai kutoka hadharini kimeonesha ukomavu wake na uzalendo kwa chama chake ambacho kimeweka wazi kuwa mtu anapokosea anaowajibu wa kujikosoa, kujishusha na kisha kuomba radhi.
"Kwahiyo na mimi naungana naye kumuombea radhi kwa Rais na Mungu ili aweze kuwamehewa," amesema
Aidha amesema anawaomba wanachama wengine watakaotambua kuwa wamekosea kutoka hadharini na kuomba msamaha.
Post a Comment