Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mhandisi Said Malik Said Kutoka Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) kuhusu ujenzi wa mradi wa Kituo cha Afya Kendwa, alipoweka jiwe la msingi la kituo hicho Wilaya ya Mkoani, Pemba Januari 09, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mhandisi Said
Malik Said Kutoka Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) kuhusu maendeleo ya ujenzi
wa mradi wa Kituo cha Afya Kendwa, alipoweka jiwe la msingi la kituo hicho
Wilaya ya Mkoani, Pemba Januari 09, 2022 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
...........................
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi na watendaji wanaosimamia miradi ya
ujenzi waongeze kasi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwapa fursa
wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Ametoa
wito huo leo mchana (Jumapili, Januari 9, 2022) wakati akizungumza na mamia wa
wakazi wa Jimbo la Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba mara baada ya kuweka jiwe la
msingi la ujenzi wa kituo cha afya cha shehia ya Kendwa ikiwa ni sehemu ya
shamrashamra za sherehe ya miaka 58 ya Mapinduzi Zanzibar.
"Nitumie
fursa hii kuwaomba viongozi na watendaji wanaosimamia mradi huu waendelee
kushirikiana na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kukamilisha ujenzi huu kwa
wakati uliopangwa ili kuwapa fursa wananchi wafaidi matunda ya mapinduzi
matukufu ya Zanzibar."
Pia
amewataka viongozi wa shehia hiyo washirikiane na Wizara ya Afya kuhakikisha
majengo na miundombinu iliyowekwa inatunzwa vema ikiwemo vifaa
vitakavyonunuliwa sasa kwa matumizi ya sasa na baadaye.
Amewataka
watumishi watakaopangiwa kuishi kwenye nyumba ya daktari wa kituo hicho,
wayatunze majengo hayo lakini pia wapande miti na kutunza mazingira
yanayowazunguka.
Akizungumzia
uboreshaji wa huduma za afya, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar ni kujenga vituo vingi zaidi ili wananchi wasiende umbali mrefu
kutafuta huduma hizo.
"Ninawasihi
tuiunge mkono nia njema iliyoonyeshwa na Mheshimiwa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali
Mwinyi."
Waziri
Mkuu ambaye kabla ya kuweka jiwe la msingi alikagua majengo matatu ya kituo
hicho, amesema ameridhishwa na ujenzi wake na hasa kiwango cha ubora kilichopo.
"Nilipofika,
nimekagua majengo kwenye zote kuanzia chini hadi juu. "Naipongeza kamati
ya usimamizi wa ujenzi wa kituo hiki kwa kusimamia vizuri ujenzi wa kituo hiki.
Ninaziagiza Kamati nyingine hapa nchini, ziige mfano wa Kamati hii ya Kendwa.
Niliposikia fedha iliyotumika sikuamini. Fedha kidogo lakini imetoa majengo
mazuri yenye viwango."
Mapema, akitoa
taarifa ya ujenzi wa kituo hicho, Msimamizi Mkuu wa Majengo kutoka ZBA,
Mhandisi Said Malik Said alisema ujenzi wa kituo hicho unaofadhiliwa na Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ulianza Agosti 28, mwaka jana na unatarajiwa
kukamilika Februari 27, mwaka huu.
"Gharama
za ujenzi ni shilingi milioni 388 lakini hadi sasa zimetumika shilingi milioni
270. Kitakapokamilika, kituo kitakuwa na majengo ya OPD, maabara, chumba cha
daktari, vyoo, chumba cha kumfanyia mgonjwa uchunguzi wa awali, chumba cha
sindano na kufunga vidonda, kitengo cha meno, wodi ya akinamama wajawazito na
nyumba ya daktari yenye uwezo wa kuchukua watumishi wawili kwa pamoja (2-in-1).
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga alisema kutokana na mabadiliko ya
sheria, ujenzi wa kituo kama hicho utaendelea kwenye shehia zote.
Alisema
kutokana na uhakiki wa walengwa wote uliofanyika Julai 2020 hadi Januari 2021,
kaya 1,992 zilisema zinaishukuru Serikali na kwa hiyari yao, zikaamua kujitoa
rasmi kwenye mpango wa TASAF wa kuhudumia kaya maskini.
"Kupitia
uhakiki huo, kaya nyingine 211,800 zimekiri kuondokana na hali duni, na kwa
hiyo, wako tayari kujitoa kwenye mpango huo baada ya miezi sita. Kutokana na
uimarishaji lishe, afya na elimu, uandikishaji shuleni umeongezeka na
mahudhurio pia yameongezeka."
Amesema
watoto wengi waliosaidiwa na mpango huo, walipata matokeo mazuri ya ufaulu wa
daraja la kwanza hadi la tatu. "Matokeo yake, watoto 782 waliohitimu mwaka
jana, wamechaguliwa kwenda vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini. Na hawa
wamesaidiwa kupata ufadhili wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu," alisema.
Akielezea
mafanikio mengine ya mradi huo, Bw. Mwamanga alisema waliwahimiza walengwa wa
mradi huo kote nchini wawe wanatunza akiba kutokana na miradi
wanayojishughulisha nayo. "Matokeo yake, vikundi 23,000 kutoka maeneo 71,
vyenye wanachama zaidi ya 350,000 vimeweza kujiwekea akiba ya shilingi bilioni
6.9 ambapo miongoni mwao, vimeweza kukopeshana shilingi bilioni 2.6 ili waweze
kushiriki shughuli za kiuchumi."
Hafla hiyo ya uwekaji jiwe la msingi ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee na Watoto, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Wilaya za Mkoani, ChakeChake, Wete na Micheweni, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wengine mbalimbali.
Post a Comment