ACT WAZALENDO YATAKA UMOJA NA UPENDO KUDUMISHWA.

Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Juma Duni Haji wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Masoud akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam akieleza dhamira yake ni kuendelea kusimamia maridhiano ya kisiasa

....................................

NA MUSSA KHALID,DAR ES SALAAM

Chama cha Siasa cha ACT Wazalendo kimewataka wanachama na viongozi wa wa chama kuendelea kudumisha umoja,upendo na mshikamano katika kujenga Chama mbadala katika kuongoza nchi kwani watanzania wanaimani kubwa na chama hicho.

Kauli  hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Juma Duni Haji wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache baada ya kuchaguliwa na chama chake kushika wadhifa huo ambapo amesema malengo yao ni kuhakikisha  chama kinajipambanua kwa siasa za masuala muhimu ya kitaifa ya kisiasa,kiuchumi pamoja na kijamii.

Aidha Mwenyekiti huyo ametaja kipaumbele cha watakayoyatekeleza kuwa ni pamoja na kusimamia na mageuzi ya uendeshaji wa chama kisiasa,Tume huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya,kuendesha siasa za masuala  na kupigania na kutetea Haki,Umoja na Maridhiano.

‘Nitashirikiana na Makamu Mwenyekiti Zanzibar kuhakikisha kuwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar unakuwa wa haki na usawa na hili litawezekana kupitia kuandikwa kwa katiba mpya ambayo itaipa Zanzibar Mamlaka yake kamili na kuweka usawa baina ya washirika wawili wa Muungano’amesema  Duni

Awali akizungumza Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Masoud amesema dhamira yake ni kuendelea kusimamia maridhiano ya kisiasa yaliyoasisiwa na Mtangulizi wake Maalim Seif Sharif Hamad katika kupigania haki za kijamii,haki za kisiasa na ustawi wa kiuchumi kwa wananchi wote.

Amesema atahuisha utamaduni wa kukifanya chama kuwa chemuchemu ya Fikra mbadala kwa kuibua hoja na kuanzisha mijadala ya kitaifa inayopelekea kuimarishwa kwa sera na sheria mbalimbali za kitaifa zinazogusa maslahi ya moja kwa moja na wananchi.

‘Kusimamia uwajibikaji wa kitaasisi ambapo kila kiongozi wa chama wa ngazi yeyote kutoka tawi hadi taifa,watendaji wa chama na wanachama kwa ujumla wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa katiba,Kanuni na maelekezo mbalimbali ya chama’amesema Mhe Masoud

Hata hivyo amesema kuwa mambo yanayohitajika baada ya kujiunga na serikali ya umoja wa kitaifa ni pamoja kurejesha imani baina ya wananchi na serikali yao na mfumo mzima wa uendeshaji wa nchi,pia kujenga serikali yenye ufanisi na kuimarisha misingi ya utawala bora na uwajibikaji katika uendeshaji wa serikali.

0/Post a Comment/Comments